• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
NDIVYO SIVYO: ‘Kupiga maji’ si sawa na kufyatua choo kichafu

NDIVYO SIVYO: ‘Kupiga maji’ si sawa na kufyatua choo kichafu

KWENYE msala mmojawapo katika makazi ya wafanyakazi wa shirika la kibinafsi, yameandikwa maneno yafuatayo: “Tafadhali piga maji!”

Mwandishi ametumia lugha kali zaidi katika msala wa pili yamkini kwa kutoridhishwa na itikio la watumizi kutokana na maandishi ya kwanza. Hivi ndivyo ujumbe huo wa pili unavyosomeka: “Kama hujui kuosha, piga maji!”

Ingawa kauli hiyo inaeleweka kwa watumizi kuwa wanapaswa kukiacha choo kikiwa safi baada ya ‘kuenda haja’, ukweli ni kuwa msamiati wenyewe umetumiwa visivyo.

Hebu fikiri iwapo maandishi kama hayo yangenakiliwa kwenye misala ya wanafunzi wa shule ya chekechea. Je, watakua wakifahamu kuwa kupiga maji ni kufyatua choo baada ya matumizi?

Jambo hilo linanikumbusha miaka yangu ya ualimu katika shule ya msingi. Wakati huo, wanafunzi wa darasa la nane waliulizwa kueleza maana ya nahau ‘piga maji’. Zaidi ya asilimia hamsini ya wanafunzi hao walichagua kiteuzi ‘kuogelea’ kama jibu la nahau hiyo.

Yamkini msukumo wao katika kuchagua jibu hilo ulitokana na uhusishaji wa moja kwa moja wa nahau na kitendo cha kugusagusa maji katika harakati za kuogelea. Hata hivyo, ifahamike kuwa maana halisi ya nahau ni tofauti sana na maneno yaliyotumiwa kuiunda.

Sina hakika iwapo kuna msemo unaotumiwa kueleza kitendo cha kufyatua choo baada ya kwenda haja ila msamiati ‘kufyatua’ unaakisi ufafanuzi huo.

Neno hilo lina maana ya kuachia ghafla kitu kilichokazwa mfano wa mtambo wa bunduki, upinde au mtego. Fasili hii pia inajumuisha kitendo cha kuvuta na kuachia ‘kitasa’ kwenye tanki la kuhifadhi maji ya kufyatulia choo.

Nimelitumia neno kitasa kwa njia spesheli kwa maana ya mtambo mdogo kwenye tanki la choo cha kufyatuliwa ambao huzungushwa au kubofyewa na kuyafanya maji kupita kwa nguvu kwenye ‘bakuli’ la choo.

Waama, si rahisi kueleza kwa nini kitendo cha kulewa sana kikapigiwa msemo ‘kupiga maji’. Yamkini muktadha ambamo nahau yenyewe imeibuka utasaidia sana katika kueleweka kwayo.

Kuna uwezekano kuwa ni nahau ambayo hutumiwa kutania tabia ya kulewa sana. Ndivyo pia inavyotumiwa nahau ‘kuvaa miwani’ kuelezea kitendo hicho hicho cha kulewa sana.

Angalau ‘kuvaa miwani’ kunaweza pia kuchukuliwa moja kwa moja kuwa na maana ya kuvaa kifaa hicho machoni ili kuona vizuri.

Lugha za kwanza pia zina baadhi ya misemo ambayo hutumiwa kwa njia ya utani kuelezea matendo fulani.

Kwa mfano, Abagusii humwelezea mtu aliyelewa sana kuwa ‘amekunywa pombe bila kutafuna vizuri’ ijapokuwa hakika pombe haitafuniki. Alhasili, ‘kupiga maji’ ni kulewa sana bali si kufyatua choo kichafu.

…MWISHO

  • Tags

You can share this post!

Anapigwa mawe akiyageuza gorofa: Diana Marua aingia orodha...

Madiwani wa Meru wakerwa na hatua ya Gavana Mwangaza kutaka...

T L