• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Makahaba wapigania pesa za Ruto

Makahaba wapigania pesa za Ruto

Na PIUS MAUNDU

MCHANGO wake Naibu Rais William Ruto wa Sh1 milioni kwa makahaba wa mji wa Mtito Andei, kaunti ya Makueni umezua zogo baina ya makundi mawili yanayopigania pesa hizo.

Dkt Ruto aliahidi kuwasaidia makahaba hao katika juhudi zake za kudhihirisha umuhimu na ufaafu wa mfumo wake wa kuinua kiuchumi watu wa mapato ya chini.

“Undeni chama cha akiba na mikopo na mtafute mbinu mbadala za heshima za kujipatia riziki,” Dkt Ruto aliwaambia makahaba ambao walipata nafasi ya kuzungumza naye alipozuru eneo hilo miezi miwili iliyopita kwa mkutano wa kampeni.

Alitimiza ahadi yake wiki iliyopita na pesa hizo zikazua vita kati ya wanawake hao.

Zogo hilo liliongezeka wiki hii baada ya kuibuka kuwa kundi moja lilikuwa limetumia nusu ya pesa hizo bila kuhusisha wenzao.

Makahaba 46 walimlaumu Caroline Mumbua, mwanamke aliyezungumza kwa niaba ya wenzake katika mkutano na Dkt Ruto, kwa kutumia visivyo pesa hizo.

Hata hivyo kundi linaloongozwa na Bi Mumbua lililaumu kundi linalolalamika kwa kumezea mate pesa hizo.

“Naibu Rais alitoa pesa hizo kupiga jeki uchumi wa makahaba wote wa Mtito Andei, lakini Carol anagawia marafiki na jamaa zake na kutumia zinazobaki kwa miradi anayotaka bila idhini yetu,” alidai Faith Mwikali.

Bi Mumbua alisisitiza kuwa ingawa pesa hizo zilinuiwa kufaidi makahaba wote wa Mtito Andei, wanafaa kujiunga na chama hicho cha ushirika.

“Muda wa usajili umepita. Hatutambui yeyote asiye mwanachama wa chama hiki,” Bi Mumbua aliambia Taifa Jumapili.

Alikiri kwamba, ametumia nusu ya pesa hizo kugawia wenzake, kununua hema, viti na vyombo vya sauti za kukodishwa na kundi lake lakini akakanusha aliondoa baadhi ya maafisa wa kundi na kujaza nafasi zao na jamaa zake.

Taifa Jumapili imebaini kuwa, baadhi ya maafisa wa usalama katika eneo hilo ni miongoni mwa walionufaika na ukarimu wa Mumbua.

Mwanamume aliyesaidia kundi hilo kuandika maazimio ya mkutano wa kundi hilo alikiri kwamba alilipwa Sh20,000.

Bi Mumbua alisema Sh500,000 zilizobaki zitatumiwa kwa mpango wa kufaidi wanachama 38 waliosajiliwa kulingana na mpango wao.

Bi Mwikali anasisitiza kuwa baada ya kupata pesa kutoka kwa Dkt Ruto, Bi Mumbua aliwatema baadhi ya makahaba wenzake.

“Baada ya pesa kuingia katika akaunti, Carol alitutenga. Anatufukuza tunapoenda kuchukua kondomu zilizotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali tulivyokuwa tukifanya, akidai siku hizi sio kama zamani,” aliongeza Mwikali.

Kundi la Bi Mumbua linasema wanaolalamika wanachochewa na wanasiasa wa eneo hilo waliomlaumu Dkt Ruto kwa kuahidi kuwasaidia huku Bi Mwikali na kundi lake wakisema pesa hizo zimewaongezea masaibu wateja wakikataa kuwalipa wakidai naibu rais aliwapa pesa kwa niaba yao.

You can share this post!

Pixel Waite asema subira ni muhimu kwa kila msanii

Usipounga Raila hutoboi, Ngilu aonya Kalonzo

T L