• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Usipounga Raila hutoboi, Ngilu aonya Kalonzo

Usipounga Raila hutoboi, Ngilu aonya Kalonzo

Na KITAVI MUTUA

GAVANA wa Kitui, Charity Ngilu, amemwambia kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kwamba, hatakuwa kwenye serikali ijayo iwapo atagombea urais bila kuungana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bi Ngilu alimuonya Bw Musyoka asiwaamini washirika wake wanaomshinikiza agombee urais akisema, wanataka kutumia sifa zake kushinda viti mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao na hawajali maslahi yake.

Akizungumza Ijumaa katika mazishi ya Edith Malombe, mke wa aliyekuwa gavana wa Kitui, Julius Malombe, Bi Ngilu alitofautiana na wanaomtaka Bw Musyoka kugombea urais kwenye uchaguzi mwaka 2022 akisema wanachotaka ni kushinda viti vyao na kumuacha makamu rais huyo wa zamani kwenye baridi ya kisiasa.

“Unafahamu wazi kuwa ni rahisi kwa washirika wako kukusifu na kukuambia utakuwa rais wa tano wa Kenya, lakini ukweli ni kwamba, unahitaji kura za kutosha kushinda kiti hicho,” Bi Ngilu alimwambia Bw Musyoka ambaye alihudhuria mazishi hayo.

Alimuonya Bw Musyoka kujihadhari na viongozi aliodai wanamshinikiza kugombea urais kwa maslahi yao ya kibinafsi ya kuhifadhi na kushinda viti.

“Ninataka kuwa wazi nawe. Tafadhali jihadhari na wanasiasa wa chama chako ambao wamezoea kutumia mbinu ya kushinda viti wakitumia jina lako bila kujali hatima yako,” alisema Bi Ngilu.

“Wakati wabunge wa chama chako wanakupigia debe katika ngome yako ya Ukambani yenye kaunti tatu ambako unajulikana katika kila boma badala ya kukutafutia kura katika maeneo mengine, je hawataki ufeli?” Bi Ngilu alihoji.

Bi Ngilu ambaye ameunga azima ya urais ya Bw Odinga alisema, Bw Musyoka hana umaarufu wa kutosha kushinda urais akigombea urais bila kuungwa mkono na vigogo wengine wa kisiasa akiwemo Bw Odinga.

Viongozi wa Wiper waliotangulia kuhutubu kwenye mazishi hayo walikuwa wamemmiminia sifa Bw Musyoka na kumtaka agombee urais wakisema ana tajiriba ya kisiasa ya kutosha kuongoza Kenya.

Seneta Enock Wambua alionya wagombeaji wengine wa urais kutoka Ukambani kwamba, eneo hilo ni ngome ya Bw Musyoka ambaye alisema ndiye mwanasiasa mpevu zaidi katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Muungano huo unajumuisha Bw Musyoka (Wiper) Musalia Mudavadi (Amani National Congress, ANC), Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

“Hakuna shaka kamwe. Rais wa tano wa Jamhuri hii atakuwa ni Kalonzo,” Seneta Wambua aliwaambia waombolezaji.

Kauli yake iliungwa mkono na wabunge Makali Mulu (Kitui ya Kati), Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati), Daniel Maanzo (Makueni) na Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Kitui Irene Kasalu waliosema kwamba, Bw Musyoka ana tajiriba ya kutosha kuwa rais.

Bw Musyoka ambaye amekuwa akisisitiza kwamba yuko katika OKA, aliepuka mjadala huo akisema yuko tayari kuongoza nchi hii na kwamba, anafahamu changamoto zinazokumba azima yake.

You can share this post!

Makahaba wapigania pesa za Ruto

MIKIMBIO YA SIASA: Maangi kumhepa Ruto kuna tija gani kwake...

T L