• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Maseneta wataka DCI ichunguze uhusiano kati ya Pasta Ezekiel na Mackenzie

Maseneta wataka DCI ichunguze uhusiano kati ya Pasta Ezekiel na Mackenzie

COLLINS OMULO Na CHARLES WASONGA

MASENETA sasa wanataka afisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Amin Mohamed kuchunguza uhusiano kati ya Pasta Ezekiel Odero na Mhubiri Paul Mackenzie kwa lengo la kuwafungulia mashtaka.

Kwenye ripoti yao waliyowasilisha katika Seneti mnamo Alhamisi, wanachama wa kamati ya muda iliyochunguza sakata ya vifo vya zaidi ya watu 400 kutokana na itikadi kali za kidini katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, wametambua uwepo wa uhusiano wa karibu kati ya wahubiri hao.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Seneta wa Tana River Danson Mungatana, imempa Bw Mohamed makataa ya siku 30 kufanya uchunguzi huo na kuwasilisha ripoti yake katika Seneti.

“Mtu yeyote ambaye alihusika kwa njia yoyote, alisadia au kufanikisha vitendo vya kikatili vilivyotekelezwa na Mackenzie, anafaa kuchunguzwa, kwa lengo la kufunguliwa mashtaka, ndani ya siku 30,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo yenye kurasa 216 imebaini uwepo wa uhusiano kati ya Kanisa la Odero la New Life Ministries na lile la Bw Mackenzie la Good News International.

Kulingana na ripoti hiyo, uhusiano huo ulianza mnamo 2020 wakati Bw Odero alitaka kununua runinga ya Times TV iliyokuwa ikimilikiwa na Bw Mackenzie.

Inasema kuwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano (CA) Ezra Chiloba aliiambia kamati ya Bw Mungatana kwamba runinga ya Times TV ilikuwa ikipeperusha mahubiri ya Odero tangu wakati huo.

Ingawa juhudi za Bw Odero za kutwaa umiliki wa Times TV hazikufaulu na hivyo akaamua kuanzisha kampuni ya New Life Communication Ltd, iliyopewa leseni mnamo Juni 18, 2021, kupeperusha vipindi kama World Evangelism TV, mhubiri huyo aliendelea kupeperusha vipindi vyake katika Times TV.

“CA ilisema kuwa uchanganuzi wake wa vipindi vya Times TV kuanzia Januari hadi Aprili 2023 ulionyesha kuwa haikupeperusha vipindi vyovyote kutoka kwa Mackenzie kwa sababu vipindi vyote vilikuwa vya Pasta Ezekiel,” ripoti hiyo inasema.

Lakini, Bw Odero alipofika mbele ya kamati hiyo, majuma mawili yaliyopita, alikana kuwa na uhusiano wowote na Bw Mackenzie.

Alisema alianza kumuona Bw Mackenzie akihubiri kwenye runinga 2010 lakini hajawahi kuhubiri pamoja naye na haungi mkono mafunzo yake ya kiajabu kama vile, kutowapeleka watoto shuleni, kususia chakula hadi mtu kufa, na dhana yake ya mafundisho ya nyakati za mwisho.

Bw Odero alisema uhusiano wake wa kipekee na Mackenzie ulikaribia wakati alitaka kununua Times TV kwa Sh3.5 milioni.

Lakini hata baada ya kulipa Sh500,000 mwanzoni, mpango huo ulitibuka alipokosa kulipa Sh3 milioni zilizosalia na ndipo “biashara” hiyo ikasambaratika.

Ripoti hiyo inasema Bw Mackenzie hakuwa na ushirikisha na viongozi wa kidini katika eneo hilo na Kaunti ya Kilifi kwa ujumla. Hii ni kwa sababu walipinga mafunzo yake ya kiajabu kuanzia 2017.

Miongoni mwa imani na mafunzo hayo ni kupinga elimu ya kisiasa, kutoa mafunzo ya itikadi kali kiasi cha kuwashauri kujiuzulu kutoka kwa kazi zao na kujiunga na kanisa lake na kupinga huduma za kimatibabu za kisasa.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Mkuu wa Italia amtema mchumba wake kwa kauli zake za...

Wito viongozi wa Mlima Kenya waungane kwa manufaa ya...

T L