• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mauti Shakahola ni unyama uliopangwa – Kindiki

Mauti Shakahola ni unyama uliopangwa – Kindiki

ALEX KALAMA Na FARHIYA HUSSEIN

HUKU awamu ya pili ya shughuli ya kufukua makaburi ili kutoa miili ya waliozikwa kwa njia tatanishi katika msitu wa Shakahola ikianza tena Kaunti ya Kilifi mnamo Jumanne, Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki amefichua kuna idadi kubwa ya makaburi.

Prof Kindiki aliyewasili kwenye msitu huo ili kuanzisha rasmi awamu ya pili ya ufukuzi maiti katika shamba linalodaiwa kumilikiwa na mhubiri tata Paul Mackenzie, amesema kuwa serikali itatumia rasilimali zote zilizopo ili kubaini kilichotokea Shakahola.

Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki (aliyevaa suti) amefichua kuna idadi kubwa ya makaburi ndani ya msitu wa Shakahola. PICHA | KEVIN ODIT

Waziri amesikitika mauaji ya Shakahola yanaingia kwa historia kuwa miongoni mwa maafa makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya.

Kufikia mwisho wa awamu ya kwanza watu 112 walikuwa wameangamia kwa sababu ya kukosa chakula na maji huku wengine wakiaga kwa kukosa hewa safi ya oksijeni “wakiamini watakutana na Yesu.”

“Nahofia kwamba kuna makaburi zaidi yanayofaa kufukuliwa. Haya matukio yanaashiria kuwa ni mauaji yaliyopangwa,” amesema waziri Kindiki.

Vilevile waziri huyo ameongezea kuwa kufikia leo Jumanne saa saba mchana, makaburi 20 zaidi yalikuwa yanafukuliwa.

Awamu ya pili ya shughuli ya kufukua makaburi ili kutoa miili ya waliozikwa kwa njia tatanishi katika msitu wa Shakahola imeanza tena Kaunti ya Kilifi mnamo Jumanne, Mei 9, 2023. PICHA | KEVIN ODIT

Kulingana na waziri huyo, bado kuna safari ndefu kwani vitengo mbalimbali vya usalama vinashughulika ndani ya chaka la mauti la Shakahola.

“Tumeongeza maafisa zaidi wakiwemo wa kutoka kitengo cha mbwa wa kunusa ili kuhakikisha shughuli hii inafanyika vizuri. Na mimi nawaahidi hakuna mtu atakayeachwa ndani ya msitu kwani tutahakikisha ya kwamba wote tumewapata,” amesisitiza.

Aidha Kindiki amesema kuwa, wakati utumiaji wa ndege katika utafutaji na uokoaji utakuwa mdogo, vyombo vya usalama vitatumia ndege zisizo na rubani, ambazo tayari zimeonekana kuwa muhimu.

Kufikia wakati waziri Kindiki alipohutubia vyombo vya habari Jumanne, vikosi vya usalama vilikuwa vimewaokoa watu wawili zaidi, na kufanya jumla ya watu waliookolewa kufikia 65.

“Tangu kuanza kwa operesheni hii hadi sasa, watu 25 wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na watakabiliwa na mashtaka mbalimbali mahakamani,” amesema.

Waziri Kindiki anezitaka familia ambazo jamaa zao wamepotea kuripoti katika kituo cha usaidizi ili kutambuliwa kwa urahisi. Wakati huo huo, amri ya kutotoka nje ya Shakahola kuanzia jioni hadi alfajiri inaendelea kutekelezwa, huku waziri Kindiki akionya kwamba yeyote atakayekamatwa nje ya saa za kutotoka nje atachukuliwa kama mshukiwa.

  • Tags

You can share this post!

Askofu Oginde aapishwa rasmi kuongoza EACC

Mkurugenzi taabani kwa kulaghai Jimi Wanjigi shamba

T L