• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Muuzaji ngozi taabani kwa kuhepa polisi miaka 3

Muuzaji ngozi taabani kwa kuhepa polisi miaka 3

Na RICHARD MUNGUTI

BAADA ya kuwahepa polisi kwa miaka mitatu hatimaye muuza ngozi nchi za ng’ambo alisukumwa miaka miwili jela.

Claire Marisiana Odimwa aliyekamatwa Aprili 5, 2023 kutoka kwa pango aliyojitengenezea katika nyumba yake mtaani Buruburu alifungwa na hakimu mwandamizi Martha Nanzushi.

Claire alifungwa kwa hatia ya kumlaghai Thomas Aul Ewald Sh4.9 milioni akimdanganya alikuwa anapeleka jamaa yake ng’ambo kwa matibabu.

Mbali na kesi hiyo, Claire anakabiliwa na shtaka lingine la kuilaghai serikali Sh204 milioni kwa kupunguza uzani wa ngozi za ng’ombe alizokuwa anasafirisha kuuza ng’ambo.

Claire alinyimwa dhamana katika kesi hii ya kuinyima serikali kodi.

Claire alihepa korti 2019 kisha polisi wakaanza kumsaka kwa udi na uvumba.

Bahati ilisimama walipomkuta Claire amejificha ndani ya kabati maalum aliyounda chini ya ngazi ndani ya nyumba mtaani Buruburu Nairobi.

Polisi aliyechunguza kesi zinazomkabili Claire alisimulia kortini vile walimkamata mshtakiwa.

“Mshtakiwa alikuwa na mazoea ya kuzima simu na kuifungua. Tulifuata masafa ya simu yake alipoipokea. Ilituelekeza hadi Buruburu,” Bi Nanzushi alielezwa.

Mahakama ilifahamishwa masafa ya simu yalitua katika makazi yake Buruburu lakini walipoingia ndani ya nyumba walimsaka hata katika dari na hawakumpata.

Lakini masafa ya simu yalionyesha angali hapo ndani ya nyumba.

“Tuliamua kuangalia ndani ya kabati iliyokuwa imefungwa katika panda ngazi hiyo. Salaala tulimpata ameketi mle ndani. Tulimkamata na kumpeleka kituo katika cha polisi,” afisa huyo wa polisi alisimulia.

Bi Nanzushi alifahamishwa na polisi kwamba “walimsaka Claire kwenye dari lakini hawakufanikiwa kumpata.”

Mshtakiwa alielezwa na hakimu kwamba alipokuwa hafiki kortini kesi ya ulaghai wa Sh4.9 milioni ilisikizwa na kuamuliwa.

Mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka miwili ama alipe faini ya Sh300, 000.

Claire alipelekwa tena mbele ya hakimu mwandamizi Bi Wandia Nyamu ambaye aliagiza apelekwe mbele ya hakimu Gilbert Shikwe anayesikiza kesi ya kusababisha nchi ipoteze kodi ya Sh204 milioni.

Katika kesi hiyo Claire anadaiwa alipunguza uzito wa ngozi za ng’ombe zilizouzwa nje kati ya 2015 na 2016.

Alipunguza uzani wa ngozi hizo kwa kilo 3, 862, 264 zilizopelekea serikali kupoteza ushuru wa Sh204 milioni.

Bi Wandia alikataa kumwachilia mshtakiwa kwa dhamana akimweleza dhamana ya zamani ilitwaliwa na serikali.

“Hakuna dhamana yoyote uko nayo. Ile ulipewa uliposhtakiwa ilitwaliwa na serikali ulipowacha kufika kortini,” Bi Nyamu alimweleza mshtakiwa.

Alipofikishwa mbele ya Bw Shikwe mnamo Aprili 14, 2023 Claire aliamriwa azuiliwe hadi kesi hiyo ya kuifanya serikali ikose ushuru wa Sh204 milioni isikizwe na kuamuliwa.

Kesi hiyo itaanza kusikizwa Aprili 28, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Mwanasaikolojia Faith Gichanga ataka kampuni, watu binafsi...

Ufungaji Tata Shakahola: Watu wengine 7 wazuiliwa Malindi

T L