• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mvua ya El Nino iko njiani, wataalamu watahadharisha Afrika Mashariki

Mvua ya El Nino iko njiani, wataalamu watahadharisha Afrika Mashariki

NA WAWERU WAIRIMU

NCHI ambazo zipo katika ukanda wa Afrika Mashariki zimetakiwa kuibuka na mikakati ya dharura ya kuzuia vifo, uharibifu wa mali na kuzuia athari za mafuriko huku mvua ya El Nino ikitarajiwa kati ya Oktoba na Desemba.

Taarifa ya Idara ya Hali ya Hewa ya nchi zilizopo katika ukanda wa Muungano wa Kiuchumi wa IGAD maarufu kama ICPAC inaonyesha kuwa mvua hiyo ya masika itakuwa ikinyesha kwa muda wa mwezi moja unaokuja.

Mvua hiyo inatarajiwa kunyesha Kusini mwa Ethiopia, Mashariki mwa Kenya na Kusini mwa Somalia na itakuwa ikiandamana na kijibaridi kikali.

“Kuna dalili kubwa kuwa mvua itanyesha sana katika sehemu kubwa ya nchi hizo za EAC na kuna uwezekano wa kutokea kwa mafuriko makubwa,” ikasema taarifa hiyo iliyotolewa mnamo Jumanne.

Ingawa hivyo, maeneo kama Kusini Magharibi mwa Uganda na Kusini Magharibi mwa Sudan Kusini ambayo yapo kame kwa sasa pia yatapokea mvua hiyo mwishoni mwa Oktoba.

Mvua hiyo kubwa hata hivyo, huenda ikaanza kuchelewa kunyesha Kaskazini mwa Somalia, Magharibi mwa Kenya, Uganda, Burundi na sehemu ya Tanzania kwa mujibu wa utabiri wa ICPAC.

Elnino hutokea wakati ambapo maji kwenye bara ya Pasifiki Pwani mwa taifa la Peru, huchemka, huzua joto na kubadilisha hali ya hewa katika nchi mbalimbali ulimwenguni. Hali hii ndiyo husababisha mvua kubwa ukanda wa Afrika Mashariki hasa kuanzia Oktoba-Novemba na Desemba.

“Kwa sasa dalili za El Nino zimeanza kuonekana ukanda wa Afrika Mashariki huku kijibaridi kikishuhudiwa maeneo mbalimbali. Baada ya miaka mitatu ya ukame, mvua hii huenda ikawa baraka kwa wakulima na kwa upande mwingine janga kwao,” akasema Mkurugenzi wa ICPAC Guleid Artan, ambaye alionya kuwa huenda vifo vikawa vingi kama tahadhari haitakwepo.

Mvua hiyo inatarajiwa itasambaratisha uchumi wa Afrika Mashariki ambao tayari upo chini kutokana na athari ya virusi vya corona na uliathirika na ukame baya zaidi ndani ya miongo minne.

Matatizo mengine ni kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vyakula ambao unatokana na vita kati ya Ukraine na Urusi na sasa watu milioni 60 wanakabiliwa na njaa. Kule Somalia, ukame ulisababisha vifo vya watu 43,000 mnamo 2022 kutokana na ripoti ambayo ilitolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mafuriko yaliyotokea Mei eneo la Beledweyne nayo yaliwaacha watu 250,000 bila makao.

Kutokea kwa El Nino kutaharibu mambo zaidi katika nchi zitakazoathirika ambazo zinaandamwa na mkurupuko wa maradhi mbalimbali pamoja na utapiamlo kwa sababu ya ukosefu wa chakula cha kutosha. El Nino mbaya zaidi ilitokea mnamo 1997/98 ambapo watu 300 walifariki na kukawa na uharibifu mkubwa wa mali na pia miundomsingi kutokana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN).

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto aongoza nchi kupongeza Faith Kipyegon na...

Ruto: Raila atatulizwa na ofisi ya upinzani

T L