• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Rais Ruto aongoza nchi kupongeza Faith Kipyegon na wanariadha walioletea Kenya medali

Rais Ruto aongoza nchi kupongeza Faith Kipyegon na wanariadha walioletea Kenya medali

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto ameongoza taifa kupongeza wanariadha walioiletea Kenya medali mbalimbali katika mashindano ya Budapest, Hungary.

Mnamo Jumamosi usiku, Agosti 27, 2023 bingwa wa mita 1500 na 5000 Faith Kipyegon alishinda dhahabu ya pili katika riadha ya mita 5000 katika mashindano hayo.

Faith 29, alitimka kwa muda wa dakika 14 na sekunde 53.88, akifuatwa kwa karibu na Sifan Hassan wa Dutch, dakika 54 na sekunde 54.11 na kujizolea nishani ya fedha.

Nafasi ya tatu ilitwaliwa na Mkenya, Beatrice Chebet aliyezoa shaba kwa muda wa dakika 14 na sekunde 54.33.

Beatrice Chebet. PICHA|HISANI

Faith Kipyegon aliibuka kidedea katika mbio za mita 5000, ikizingatiwa kuwa alitoana kijasho na wanawake wengine kumi wenye kasi zaidi.

“Faith Kipyegon, mwanariadha machachari, hodari na wa kipekee amezoa dhahabu ya pili katika Mashindano ya Kimataifa ya Budapest mita 5000. Isitoshe, Emanuel Wanyonyi riadha za mita 800 wanaume na Beatrice Chebet mita 5000 wanawake wamezoa fedha na shaba, mtawalia,” Rais Ruto akapongeza.

Mnamo Jumanne, Agosti 22, 2023, Faith alitia kapuni dhahabu ya kwanza katika riadha za mita 1500.

Emanuel Wanyonyi. PICHA|HISANI

Wengine waliomiminia sifa wanariadha hao wa Kenya ni Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga, miongoni mwa viongozi wengine wakuu serikalini na wanasiasa.

“Mwaka huu, umekuwa wenye baraka kwangu,” Faith akasema baada ya kuibuka kidedea Budapest.

Mwanariadha huyo ameshinda dhahabu mara mbili Olimpiki, katika mbio za mita 1500.

Mwaka huu, 2023 ameandikisha rekodi mpya katika masafa ya mita 1500 na mita 5000.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mzozo wa Malisho: Wakazi wa Vitengeni, wafugaji washikana...

Mvua ya El Nino iko njiani, wataalamu watahadharisha Afrika...

T L