• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2024 2:01 PM
Mwana wa waziri wa zamani mashakani kwa vitisho vya kuua

Mwana wa waziri wa zamani mashakani kwa vitisho vya kuua

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAWE aliyekuwa naibu waziri wizara ya biashara ameshtakiwa kutisha kumuua mfanyabiashara aliyempora Sh50 milioni.

Musaari Kahiga Syongoh, mwanawe Zaddock Syongoh alikabiliwa na mashtaka mbalimbali ya kutisha kuua, kujifanya afisa wa ujasusi na kupatikana na misokoto tano ya bhangi

Musaari alishtakiwa pamoja na msaidizi wake mkuu (PA) Alvin Nzomo Muthami kwa kutisha kumuua Chetan Babu Jamnadas Gohil kati ya Septemba 1, 2022 ba Mei 11, 2023.

Kupitia kwa wakili Moses Chelang’a wawili hao waliomba waachiliwe kwa dhamana.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Abel Omariba na wakili Ken Odera anayemwakilisha Gohil kwa madai wakiachiliwa “watatekeleza vitisho vyao na kumuua mlalamishi Chetan Babu Jamnadasi Gohil almaarufu CJ.”

Alisema Omariba, “Polisi wamepokea habari kwamba Musaari anaendelea na mipango ya kununua bunduki aina ya AK47 atakayotumia kumuua Gohil.”

Omariba aliomba mahakama iwazuilie wawili hao hadi pale Gohil atakapotoa ushahidi.

“Gohil anahofia maisha yake. Naomba hii mahakama iwazuilie washtakiwa hadi pale Gohil atakapotoa ushahidi,” Omariba alimsihi hakimu.

Musaari aliyewania kiti cha ubunge cha Lang’ata na kushindwa, pia alisemekana atatekeleza vitisho vyake.

Chelang’a alimwomba hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Zainabu Abdul awaachilie Musaari na Nzomo kwa dhamana akisema “hawatatoroka.”

Hakimu alielezwa polisi wamekuwa ‘wakitembeza’ madai hayo ya vitisho na hayana msingi.

Wawili hao walikabiliwa na mashtaka manane.

Nzomo alishtakiwa peke yake kwa kutuma jumbe za vitisho kwa Gohil na kupatikana na vitambulisho vya watu wengine katika mtaa wa Donholm Nairobi.

Nzomo pia alishtakiwa kwa kutekeleza uhalifu wa kimitandao kwa kumtumia jumbe za vitisho Gohil.

Hakimu aliamuru washtakiwa hao wazuiliwe hadi Jumatatu, Juni 12, 2023 katika kituo cha polisi cha Parklands wahojiwe na afisa wa urekebishaji tabia, ndipo aamue ikiwa atawaachilia kwa dhamana au la.

 

  • Tags

You can share this post!

Talanta Hela: Akothee alalamika baada ya kumwaga unga

Wahuni waliopora wanandoa wa China mamilioni Juja wasakwa  

T L