• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wahuni waliopora wanandoa wa China mamilioni Juja wasakwa  

Wahuni waliopora wanandoa wa China mamilioni Juja wasakwa  

NA SAMMY WAWERU

MAKACHERO wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI) Juja, Kaunti ya Kiambu wanasaka genge la wahuni watano, walionyang’anya wanandoa kutoka China kima cha Sh4 milioni pesa taslimu.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, DCI imechapisha picha ya mmoja wa wezi hao ikiomba umma kumripoti mara moja pindi atakapoonekana.

Uhalifu huo ulitekelezwa mnamo Jumamosi, Juni 10, 2023, katika kile kinaashiria kama njama iliyopangwa.

Kulingana na DCI, wahalifu watatu kati ya tano wanaosakwa walikuwa wamevalia sare rasmi za polisi.

“Makachero wa DCI Juja, wanatafuta mshukiwa huyu ambaye tumechapisha picha yake kufuatia wizi uliofanyika jana (Jumamosi) eneo la Juja, Kiambu,” inasema taarifa ya idara hiyo.

Wanandoa hao wanasemekana kutoa fedha walizoporwa (Sh4 milioni) kwenye benki, Chiromo, Nairobi kabla kuelekea Kiahuria, Juja.

Wanaendeleza biashara ya machimbo Juja, wasijue walikuwa wamefuatwa na genge la wezi lililowasimamisha katika barabara ya Bob Haris.

“Gari jeupe aina ya Toyota Axio, nambari za usajili KDD 189P lilisimamisha lao, wakaingia ndani kwa nguvu na kutoweka na pesa,” DCI ikaarifu.

Mshukiwa ambaye picha yake imechapishwa mitandaoni japo majina yake hayajabainika, anaonekana amevalia jaketi nyeusi, shati la kahawia na kofia nyeusi ya chepeo.

Visa vya wizi wa nguvu za kimabavu, hasa baada ya kutoa pesa benkini vimeandikisha kuongezeka nchini wahudumu wa benki wakitajwa kushirikiana na wahuni.

Wizi wa kimitandao, unaohusisha kadi za simu na za benki pia umeongezeka.

  • Tags

You can share this post!

Mwana wa waziri wa zamani mashakani kwa vitisho vya kuua

Mamake Trio Mio aomba msaada wa DCI mwanawe akitishwa kuuawa

T L