• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ndoa za mitara zitatatua changamoto Mlimani – Wanguku

Ndoa za mitara zitatatua changamoto Mlimani – Wanguku

NA MWANGI MUIRURI

MWENYEKITI wa Kongamano la Wanaume wa Agikuyu almaarufu Men’s Conference Bw Thuo Mathenge amesema wakazi wa eneo hilo wanahitaji kukumbatia ndoa za wake wengi, yaani ndoa za mitara.

Bw Mathenge ambaye kwa ulingo wa siasa anafahamika kama Wanguku kutokana na biashara yake ya ufugaji wa kuku, analalama kwamba eneo hilo liko hatarini ambapo wakazi wengi wamezama kwa ulevi na hata mafundisho tata ya kidini.

Alisema ulevi ni chanzo cha wengi kutowajibika huku dini ikipotosha watu kwamba ndoa ya wake wengi ni ushetani.

Amesema kwamba “tunafaa kuiga hizi jamii za Kaskazini Mashariki ambazo wengi ni Waislamu wanaofundishwa kwamba mwanamume anaweza akaoa wanawake wanne.

Bw Mathenge kwenye mahojiano na kituo cha runinga cha Inooro, alisema kwamba ataitisha mkutano mkubwa katika uwanja mmoja wa eneo hilo na kutolewe kauli mbiu ya ndoa kwa wake wengi.

Alisema ni aibu kubwa jamii iliyokuwa ikijivunia ubabe kupindukia wa idadi ya watu kuanza kutishiwa wingi huo na jamii za kuhamahama.

“Hata wakazi wa Mlima Kenya wenye mali walio na mke mmoja mmoja wanapanga uzazi kudhibiti idadi ya watoto iwe ndogo badala ya kujaza dunia. Mimi nina watoto zaidi ya 10 na nitazidi kuwaongeza katika kila pembe ya eneo hili,” akasema.

Aliwataka wanaume wa jamii hiyo watie bidii kujijenga nguvu za kiume “ili mjipe ushujaa wa kuzalisha watoto wengi kwa mpigo kama ndugu zetu wa Magharibi”.

Alisema shule za eneo hilo zinazidi kufungwa kwa kukosa wanafunzi huku vijana wa eneo hilo wakibakia na mbegu mwilini.

“Tusiwe wajinga wa kusema kwamba kuna shida ya pesa. Eti hujui ukioa wanawake wengi utalemewa na malezi. Ukienda Kaskazini Mashariki kwenye familia moja unapata kuna zaidi ya watoto 20 na ni jangwani. Jipeni moyo kwamba mko katika eneo la rotuba na watoto watapata neema ya Mungu na wanawake pia,” akasema.

Hata hivyo, ni vyema ieleweke kwamba Bw Wanguku ni bilionea aliye na kampuni zaidi ya 10 zinazompa mapato huku akisalia na pesa za ziada za kusukuma kampeni za kuwania ugavana wa Kaunti ya Nyeri ingawa hajafanikiwa tangu 2013.

  • Tags

You can share this post!

Ushoga: World Bank yauma miradi ya umma Uganda

Wizara ya Ardhi haijafanya hamasisho la mfumo wa kidijitali...

T L