• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Ni fahari kuona Mudavadi akiinuliwa, asema Gachagua

Ni fahari kuona Mudavadi akiinuliwa, asema Gachagua

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua, Ijumaa, Oktoba 6, 2023, amesema kuwa hana shida yoyote na hatua ya Rais William Ruto kumkweza kimamlaka Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Bw Gachagua alisema kwamba badala yake, amekuwa akimrai Rais Ruto kumpunguzia baadhi ya majukumu ambayo amempa.

Kwenye mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyofanya Jumatano usiku, Rais Ruto alionekana kumkweza kimamlaka Bw Mudavadi, kwa kumpa Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Ni hatua iliyofasiriwa kama tishio la kisiasa kwa nafasi, usemi na ushawishi wa Bw Gachagua katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Mimi na Rais Ruto ni marafiki. Huwa tunashauriana kuhusu kila jambo tunalofanya. Nimepewa majukumu mengi sana. Kwa kweli, hata nimekuwa nikimrai anipunguzie baadhi ya majukumu aliyonipa,” akasema Bw Gachagua, akishiria kwamba walikuwa wameshauriana na Rais kuhusu hatua ya kumkweza Bw Mudavadi.

Bw Gachagua alisema hayo Ijumaa asubuhi, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, katika makazi yake mtaani Karen, jiji Nairobi.

Kauli yake ilijiri siku moja tu baada ya baadhi ya viongozi katika ukanda wa Mlima Kenya kukosoa mabadiliko hayo, wakiyataja “kulipendelea” eneo la Magharibi.

Mnamo Alhamisi, Gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Gachagua, alikosoa mabadiliko hayo, akisema “yanatoa ujumbe fulani kwa Mlima Kenya ielekeapo 2027.

Hata hivyo, Bw Gachagua alitofautiana na gavana huyo, badala yake akisema kuwa mabadiliko hayo hayakulilenga eneo la Mlima Kenya kwa namna yoyote ile.

“Nafasi zilizotengewa Mlima Kenya bado zipo. Hazijachukuliwa na watu wengine. Hivyo, watu wetu wanafaa kutulia, kwani mgao wetu katika serikali hii bado upo,” akaeleza.

Naibu Rais pia alikanusha uwepo wa tofauti yoyote baina yake na waziri mpya wa Utumishi wa Umma, Bw Moses Kuria.

“Bw Kuria ni kama mtoto wangu. Kile tulifanya ni kumlainisha tu kimienendo, kama baba afanyavyo kwa watoto wake,” akasema.

Bw Gachagua pia alisema amefanikiwa kupata wafanyabiashara kutoka nchi za Amerika na Milki ya Kiarabu (UAE) watakaonunua kawaha kutoka kwa wakulima moja kwa moja.

“Tumeanza kuona mwanga kwenye juhudi zetu za kulainisha masuala ya kahawa. Wakulima wataanza kutabasamu hivi karibuni,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi wauza matikitimaji kufidia hasara ya samaki kuoza...

Daktari athibitisha mwanamume aliyefariki baada ya kunywa...

T L