• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Operesheni yaanika wanaotumia ethanol kutengeneza pombe hatari

Operesheni yaanika wanaotumia ethanol kutengeneza pombe hatari

NA TITUS OMINDE

KAMPENI ya serikali dhidi ya pombe haramu Kaunti ya Uasin Gishu imefichua wafanyabiashara wanaotumia kemikali ya ethanol kutengeneza pombe hatari kwa afya ambayo haikidhi viwango vinavyohitajika.

Polisi walisema wanafuatilia wafanyabiashara katika mji wa Eldoret na viunga vyake ambao wanatumia kemikali hiyo katika utengenezaji na kupakia pombe hiyo haramu katika chupa za pombe zenye chapa.

“Hili ni jambo la kutia wasiwasi sana. Watengenezaji pombe haramu sasa wanachanganya na kemikali ya  ethanol. Sisi maafisa wa serikali hatutakubali,” alisema naibu kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Turbo Chris Wesonga.

Akizungumza baada ya kuwakamata wanaume wawili wenye umri wa kati ya miaka 19 na 24 katika barabara kuu ya Eldoret-Webuye walipokuwa wakisafirisha shehena yenye madumu 55 ya lita 20 za kemikali ya ethanol kwa mfanyabiashara wa Eldoret, Bw Wesonga alisema wafanyabiashara wa pombe haramu ambao wanatumia ethanol wameamua kuajiri vijana wa kuwasafirishia pombe hiyo ili kuficha uovu wao.

Polisi pia walifichua kuwa wafanyabiashara wa pombe hiyo sasa wanahamia mitaa ya kifahari ili kuficha biashara yao haramu.

Mnamo Jumatatu, polisi walipokamata washukiwa hao walinasa shehena ya ethanol ya kima cha Sh600,000 inayoshukiwa kuwa ilitoka nchi jirani.

Akithibitisha kisa hicho Bw Wesonga alisema wamekamata gari la Toyota Sied lililokuwa likitumiwa kusafirisha kemikali hizo haramu.

“Tunamshikilia dereva na msaidizi wake ambao sasa wanasaidia polisi kufanya uchunguzi. Maafisa wetu wameanzisha msako wa kumtafuta mmiliki wa shehena hiyo kabla ya kuwapeleka wote mahakamani kwa kujihusisha na biashara haramu,” akasema Bw Wesonga.

Hii ilikuwa baada ya polisi kufahamishwa na wananchi kwamba gari hilo lilikuwa limebeba kemikali za magendo kutoka nchi jirani likielekea mjini Eldoret.

“Dereva na mwenzake walipopuuza agizo la kusimama eneo la Lumakanda. Wenzetu waliwaarifu maafisa wetu wanaosimamia kizuizi cha barabara katika kituo cha biashara cha Juakali kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye ambapo waliwekewa mtego,” alisema Bw Wesonga.

  • Tags

You can share this post!

Cesc Fabregas aangika daluga, sasa ndiye kocha wa Como...

AMINI USIAMINI: Pacu ni samaki mwenye meno kama ya binadamu

T L