• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Cesc Fabregas aangika daluga, sasa ndiye kocha wa Como nchini Italia

Cesc Fabregas aangika daluga, sasa ndiye kocha wa Como nchini Italia

NA MASHIRIKA

KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Barcelona na Chelsea, Cesc Fabregas, 36, ameangika daluga zake katika ulingo wa usogora.

Nyota huyo mwenye umri wa mika 36 anastaafu baada ya kunyanyua Kombe la Dunia akiwa na Uhispania na mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akichezea Chelsea na Kombe la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) akivalia jezi za Barcelona.

“Nasikitika kutangaza kuwa muda wangu katika ulingo wa soka umekamilika na sasa naangika daluga,” akaandika Fabregas kwenye Instagram.

Fabregas anastaafu kwenye ulingo wa soka akisalia na mwaka mmoja kwenye mkataba wa miaka miwili kambini mwa kikosi cha Como kinachoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Italia (Serie B).

Sasa ndiye kocha wa chipukizi kambini mwa Como.

“Sasa nitaanza kuwa kocha wa kikosi cha akiba cha Como B na kile cha chipukizi. Huu ni mradi ambao napania kuchangamkia kwa moyo wangu wote,” akaelezea.

Fabregas alijiunga na akademia ya Barcelona almaarufu La Masia akiwa na umri wa miaka 10 pekee mnamo 1997. Baada ya kuwa tegemeo la akademia ya Barcelona, alisajiliwa na Arsenal waliomwajibisha mara 212 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na akasaidia kikosi hicho kushinda Kombe la FA kati ya 2004 na 2011 kabla ya kurejea Barcelona.

Baada ya kuhudumu kambini mwa Barcelona kwa miaka mitatu ugani Camp Nou, alirejea Uingereza kuchezea Chelsea mnamo 2014 na akawajibishwa na kikosi hicho karibu mara 200.

Alihamia AS Monaco baadaye na akawajibikia kikosi hicho cha Ufaransa mara 68 katika kipindi cha miaka mitatu na nusu kilichotamalakiwa na wingi wa visa vya majeraha kabla ya kuhamia Como.

Fabregas alichezea timu ya taifa ya Uhispania mara 110 na akawa sehemu ya kikosi kilichonyanyua taji la Euro mara mbili mnamo 2008 na 2012 na Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Korti kuamua kuhusu ombi la kumfunga mkuu wa EPRA

Operesheni yaanika wanaotumia ethanol kutengeneza pombe...

T L