• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Polisi akamatwa akidaiwa kuvuta bangi na kujiunga na waandamanaji

Polisi akamatwa akidaiwa kuvuta bangi na kujiunga na waandamanaji

NA MWANGI MUIRURI

AFISA wa polisi alitiwa mbaroni Alhamisi katika Kaunti ya Makueni akidaiwa kushiriki maandamano huku akiwa amejibebea misokoto 40 ya bangi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka huduma ya polisi nchini (NPS), Kobstabo Evans Otieno alikamatwa Emali katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

“Tunathibitisha kukamatwa kwa afisa huyo kupitia tukio lililonakiliwa kwa nambari OB:15/20/7/2023 saa nne na dakika 20 mchana,” taarifa hiyo ya Mkuu wa Polisi Bw Japhet Koome ikasema.

Ripoti hiyo ilisema kwamba afisa huyo alikamatwa alipokuwa akipanga waandamanaji katika kizuizi haramu cha barabarani.

“Afisa huyo alikuwa miongoni mwa raia waliokuwa wakihangaisha wenye magari kwa kuwavurumishia mawe. Aidha, imebainika kuwa afisa huyo alionekana na wenzake katika mji wa Emali akiwa miongoni mwa waandamanaji waliorusha mawe katika kituo cha polisi cha Emali,” ripoti hiyo yasema.

Alipokamatwa, maafisa wa polisi walipekua mifuko yake na ambapo ilidaiwa alipatikana akiwa na misokoto 40 ya bangi yenye thamani ya Sh2,000.

Kwa sasa, ripoti hiyo iliongeza, atafikishwa mahakamani, hatua ambayo itasababisha kusimamishwa kazi akingoja hukumu.

Iwapo ataondolewa lawama kortini, ina maana kwamba atarejeshwa kazini lakini akipatikana na makosa atafutwa kazi na apoteze marupurupu yake ya kustaafu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ruto asuta Azimio akisema sufuria kichwani haitashusha...

Fahamu kwa nini unashauriwa kula nyama ‘halal’

T L