• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Fahamu kwa nini unashauriwa kula nyama ‘halal’

Fahamu kwa nini unashauriwa kula nyama ‘halal’

NA KALUME KAZUNGU

MARA nyingi utasikia au kushuhudia biashara ya nyama haramu, ikiwemo paka, mbwa na kadhalika ikiendelezwa kwenye baadhi ya miji ya Kenya ikiwemo Nakuru, Naivasha, Nyandarua, Mai Mahiu na kwingineko.

Aghalabu vyombo vya habari hujulisha watu kuwa fulani katiwa mbaroni eti kwa sababu kapatikana akichinja mbwa, paka au wanyama wengine wasiofaa kwa minajili ya kutengeneza samosa au mishikaki kuuzia wateja.

Kuna baadhi ya miji nchini ambapo inatambulika fika kuwa hata mja kujinunulia chakula chochote kinachoambatana au kutengenezwa kutokana na nyama kama vile samosa na mishikaki ni suala la kutiliwa shaka.

Ama kwa hakika biashara ya nyama kwenye miji hiyo kaingia doa jeusi kutokana na visanga vya mara kwa mara vya uuzaji na usambazaji wa nyama za sampuli isiyofaa.

Katika kisiwa cha Lamu aidha, hali ni tofauti.

Hapa, biashara ya nyama haramu haijapenya hata.

Licha ya mji wa kale wa Lamu kudumu kwa miaka zaidi ya 700, hakuna hata siku moja ambapo nyama haramu imepenya kuuziwa wananchi kisiwani hapo.

Hapa, mlaji wa nyama kila wakati ni mwenye furaha akijua fika kuwa nyama yoyote inayomfikia mezani ni ile iliyo halali pekee.

Katu hutapata nyama ya punda, mbwa, paka na hata nguruwe ikiuzwa kisiwani Lamu, iwe ni kwa siri au paruwanja.

Taifa Leo ilichimba chini kutaka kujua ni mambo gani hasa yaliyofaulisha kisiwa cha Lamu kudhibiti kabisa ulaji au uuzaji wa nyama sampuli isiyofaa.

Kwanza ikumbukwe kuwa kisiwa cha Lamu ndicho chenye wakazi wengi wanaofuata misingi ya dini ya Kiislamu ukilinganisha na maeneo mengine nchini Kenya na hata Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Karibu asilimia 80 ya wanakisiwa cha Lamu ni Waislamu wa asili ya jamii ya Wabajuni.

Ili kudhibiti kupenyezwa na kuendelezwa kwa biashara ya nyama haramu Lamu, wenyeji hapa wameibuka na mpangilio mwafaka katika kuchinja mifugo kama vile mbuzi, ng’ombe, na kondoo.

Ni Lamu ambapo kwanza utapata vichinjio vingi na buchari za nyama zikimilikiwa au kusimamiwa na Waislamu, hali ambayo imeziba kabisa mwanya wa mwenye nia ya kuingiza nyama isiyo halali kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM) tawi la Lamu, Mohamed Abdulkadir alitaja dini na utamaduni wa watu wa Lamu kuwa changizo kuu ya kuendelezwa kwa desturi ya kuzuia kabisa biashara ya nyama haramu eneo hilo miaka nenda miaka rudi.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu (Supkem) tawi la Lamu Mohamed Abdulkadir. Anasema uhalali wa nyama kisiwani Lamu unatokana na misingi ya dini na utamaduni wa tangu jadi wa wakazi wa Lamu.
PICHA | KALUME KAZUNGU

Kulingana na Bw Abdulkadir, dini ya Kiislamu ambayo ndiyo iliyokita mizizi kisiwani Lamu imeruhusu mja kula nyama za baadhi ya wanyama, kanuni anayoitaja kuwa yenye manufaa makubwa kwa maisha ya mtu na jamii kwa ujumla.

Anasema wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi na kadhalika hawana neno kutumika na binadamu.

Anasema ni kinyume cha dini ya Kiislamu na utamaduni wa Lamu kumpata mtu akiuza au kula nyama ya paka, mbwa, nguruwe, punda na vinginevyo haramu.

“Dini ya Kiislamu imeruhusu kula nyama za baadhi ya wanyama lakini imekataza kula baadhi ya nyama za wanyama wengine kama vile mbwa na paka. Wanyama walioruhusiwa kuliwa na binadamu ukichunguza utapata wako na faida tele kiafya. Nyama zilizoharamishwa utagundua madhara yake ni mengi kiafya. Ndiyo sababu Lamu hutapata nyama yoyote iliyokatazwa katika Quran ikiuziwa waja kwani dini ya jadi hapa ni Uislamu,” akasema Bw Abdulkadir.

Kiongozi huyo wa dini anataja mfano wa nyama ya nguruwe kwamba imekatazwa kidini kutokana na aina ya ulaji wake, muonekano, maumbile ya mnyama huyo ambayo ni mabaya na kuwa na vitu vyenye madhara ambavyo vitamuathiri mwanadamu kama uwepo wa mnyoo unaojulikana kama trichina (kwenye nyama).

“Hata kwenye Quran, nguruwe ametajwa sehemu tano. Mfano wa aya ambazo zimetaja nguruwe ni ile ya Surah al-Maeda 5:3 inayosema-‘Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliyechinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu…” ananukuu Bw Abdulkadir.

Kwa upande wake, Imamu wa Kisiwa cha Lamu, Mahmoud Mau anawataka wale wanaozuru au kuishi kisiwa cha Lamu na ambao hupenda kula nyama waondoe shaka.

Nyama ikisafirishwa kwa mkokoteni spesheli kisiwa cha Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema Lamu hakuna nafasi ya nyama haramu kuuzwa sokoni au buchari yoyote ile.

Bw Mau kadhalika anasema si nyama haramu tu, hata ile halali lakini ambayo haikuchinjwa kulingana na taratibu za Uislamu ni vigumu kuipata sokoni au kwenye maduka ya nyama.

Kiongozi huyo wa dini anasema nyamafu pia haijapenya kuuzwa kisiwani Lamu kutokana na wenyeji kuzingatia mafundisho ya dini na utamaduni.

“Usisumbukie suala la nyama haramu ukiwa kisiwani hapa. Hakuna na haiwezi kupenya katu hapa. Isitoshe, hata mnyama ambaye hakuchinjwa na kumwaga damu inavyostahili hakubaliki hapa. Tangu jadi hakujashuhudiwa mbwa, paka au chochote najisi kikichinjwa na kuuzwa mjini hapa. Tuko na mpangilio wetu wa kuchinja wanyama hapa. Twasikia tu uwepo wa nyama haramu maeneo mengine ya Kenya lakini si Lamu,” akasema Bw Mau.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mbwana Shee anasema mbali na Uislamu na utamaduni, wenyeji wa Lamu pia wameweka mikakati sufufu ya kuhakikisha nyama zinazouzwa sokoni na madukani zinakaguliwa na kupasishwa vilivyo.

Kulingana na Bw Shee, kuna watu nmaalum ambao pia wamewekwa spesheli kuchinja mifugo kabla ya nyama kuuzwa kisiwani Lamu.

Isitoshe, kuna waliowekwa kichinichini kama majasusi wa jamii.

“Tuko na majasusi wetu wa kusambaza habari endapo watapata mifugo ikichinjwa isivyostahili, hasa Kiislamu. Hawa pia hupasha jamii habari endapo kuna jaribio la mnyama haramu kuchinjwa kisiwani. Hilo limewafanya wamiliki wa vichinjio na buchari kuwa makini zaidi wakijua fika kuwa endapo watashukiwa basi watakosa biashara kwani vichinjio au buchari zao zitasusiwa, hivyo nyama kuwaozea na kukadiria hasara si haba,” akasema Bw Shee.

Mzee Muhashiam Famau anasisitiza kuwa kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Quran, Mwenyezi Mungu alitahadharisha waja wake dhidi ya kujilia vyakula vivi hivi, akishikilia kuwa kwenda kinyume kuna madhara yake.

“Twajua kuwa Quran inasema yale yaliyofunuliwa Mtume wetu ambayo ni haramu kwa mlaji kutumia ni nyamafu, damu inayomwagika, nyama ya nguruwe na vinginevyo. Vyote hivyo vyahesabika kuwa uchafu. Ndio sababu hutapata biashara ya nyama haramu ikifanyika Lamu kwani hapa tumejikita katika dini ya Kiislamu na tamaduni zetu za jadi zinazotukataza mambo hayo,” akasema Bw Famau.

Kulingana na Uislamu, vitu vinaharamishwa kwa sababu nyingi; ima kwa hekima, au bila hekima ikiwa ni sehemu ya mitihani na kupimwa viumbe utiifu wao, na kwa hekima mfano ni vichafu au vina madhara.

Ikiwa kitu chochote kina madhara kinakuwa haraam; na kikiwa kina manufaa kinakuwa halal; na kikiwa madhara yake ni makubwa kuliko manufaa kitakuwa ni haram; ilhali madhara yake yakiwa ni kidogo kuliko manufaa kinakuwa ni halal.

“Uislamu umeweka aina yake ya kuchinja ambayo inamfanya mnyama atoe kiwango kikubwa cha damu. Kama tunavyojua ni kuwa damu ni chombo cha kubeba viini vya ugonjwa na kemikali ambazo zina madhara na hasa kwa mwanadamu. Kubakia ndani ya mnyama, damu huenda ikaleta madhara makubwa kwa mlaji. Na kwa sababu hiyo, nyamafu ni marufuku kwetu kwani damu nyingi hubakia ndani ya mwili wa nyamafu badala ya kutoka nje kumwagika jinsi inavyofaa wakati mnyama huyo amechinjwa kwa njia inayofaa,” anaeleza Bw Mau.

Miongoni mwa faida za Mwislamu katika kula nyama halali ni kwamba hujiepusha kupata magonjwa kiholela ikilinganishwa na nyama yoyote ile nyingine.

Ni bayana kwamba uwezekano wa kula nyama halali kisiwani Lamu kwa wale wanaopenda nyama basi ni karibu asilimia 99.

Hivyo, kwa wale akina ndugu na dada ambao wamekuwa wakikereketwa maini kila wanapofika Nakuru, Naivasha, Nyandarua, Nairobi na kwingineko wakitaka kula nyama, hamna budi ila kukimbilia kisiwa cha Lamu kwani nyama halali ndio inayokubalika.

Hakuna nafasi ya uuzaji wa nyama, samosa au mishikaki ya mbwa, paka, punda na vinginevyo najisi hapa kama inavyofanyika sehemu nyingine za nchi na ulimwengu.

  • Tags

You can share this post!

Polisi akamatwa akidaiwa kuvuta bangi na kujiunga na...

AFC Leopards kuhamisha mechi zake za nyumbani kutoka Nyayo

T L