• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Raila aagiza maandamano yaishe saa kumi na moja jioni, kuendelea kesho Alhamisi

Raila aagiza maandamano yaishe saa kumi na moja jioni, kuendelea kesho Alhamisi

WINNIE ATIENO Na KARIM RAJAN

KINARA wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, amewataka Wakenya kusitisha maandamano ya kuipinga serikali saa kumi na moja jioni.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Odinga amesema maandamano ya amani ya kupinga nyongeza ya ushuru na kupanda kwa gharama ya maisha yataanza tena asubuhi kesho Alhamisi.

Kiongozi huyo wa ODM amesema kuwa, maandamano ya leo Jumatano yamekuwa na matokeo mazuri.

“Tutaendelea na maandamano yetu ya amani kama tulivyopanga. Lakini tutayazima leo (Jumatano) saa kumi na moja jioni na kuendelea asubuhi ya kesho Alhamisi. Tutaendelea kutetea haki zetu sisi Wakenya, hatutakata tamaa,” akasema, huku akiwashukuru Wakenya kwa kumiminika barabarani kupigania haki zao.

Wakati uo huo, mwanasiasa huyo mkongwe ameelezea kushtushwa na kukamatwa kwa waandamanaji na wanasiasa wa upinzani Ken Chonga (Mbunge wa Kilifi Kusini), Teddy Mwambire (Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi) miongoni mwa wengine. Mwandishi wetu wa Kilifi amesema Stewart Madzayo (Seneta wa Kilifi) amekwepa maafisa wa polisi.

Mlinzi wa Bw Odinga, Bw Maurice Ogeta alikuwa ametekwa asubuhi lakini kiongozi huyo amethibitisha kwamba ameachiliwa huru lakini Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, bado haijulikani aliko. Bw Odinga ameagiza serikali iwaachilie viongozi wote waliokamatwa akiwemo Bw Owino.

Bw Owino alikamatwa na maafisa wa polisi Nairobi. Kwenye taarifa fupi kupitia ukurasa wake wa Twitter Bw Owino alidai kuwa alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumanne jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) alipowasili kutoka Mombasa.

Alikuwa ameenda Mombasa kushiriki mipango ya maandamano ambayo yaliitishwa na Azimio kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na viwango vya ushuru.

“Nimezuiliwa na maafisa wa DCI katika uwanja wa JKIA baada ya kuwasili kwangu kutoka Mombasa. Sasa nimekamatwa,” akasema.

Mbunge huyo ni miongoni mwa wabunge wa  Azimio kutoka Nairobi waliotarajiwa kupanga maandamano jijini Nairobi. Duru zinasema kuwa huenda Bw Owino alikamatwa ili kumzuia kuandaa mkutano katika uwanja wa Jacaranda, ulioko katika eneobunge lake la Embakasi Mashariki.

Azimio ilitaja, kwenye taarifa Jumanne kwamba, uwanja huo wa Jacaranda, uwanja wa Kamukunji na uwanja Joseph Kang’ethe, (eneobunge la Kibra) kama ambako wafuasi wake wangekutana kabla ya kuanza maandamano.

Mnamo Jumatatu, viongozi wa Upinzani walitangaza siku tatu za maandamano kuanzia Jumatano hadi Ijumaa. Kutokana na hatua hiyo serikali ilitangaza kufungwa kwa shule za kutwa za msingi na upili katika miji ya Mombasa, Nairobi na Kisumu kutokana na ukosefu wa usalama.

  • Tags

You can share this post!

Mzee adai polisi walimuumiza mgongo akitetea shamba lake

Karua alaani hatua ya maafisa kuwakamata viongozi wa Azimio...

T L