• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Mzee adai polisi walimuumiza mgongo akitetea shamba lake

Mzee adai polisi walimuumiza mgongo akitetea shamba lake

NA MAUREEN ONGALA

MWANAMUME mmoja kutoka kijiji cha Mwembe Legeza katika wadi ya Utange iliyoko eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa amelalamikia kuhangaishwa, kupigwa na polisi huku akiachwa akiuguza majeraha ya uti wa mgongo.

Bw Hamisi Said amekuwa akijipata katika mikono ya polisi mara kwa mara akilinda shamba lao lenye ukubwa wa ekari 21 lisinyakuliwe na bwanyenye mmoja anayedai umiliki wa ardhi hiyo.

Akizungumza na Taifa Leo nyumbani kwake, Bw Said alisimulia masaibu yake baada ya kukataa amri ya bwanyenye huyo ambaye alitaka kuwafurusha kutoka kwa kipande hicho cha ardhi hata bila idhini ya mahakama.

“Bwanyenye huyo amegawanya shamba letu na kuuza bila sisi kujua… ni njama aliyofanyia ofisini. Kila mara watu wake wanakuja huku na stakabadhi kutaka kutuondoa lakini tumedinda kwa sababu ni shamba la akina babu zetu,” akasema Bw Said.

Anaeleza kwamba kila mara wanapoanza kuuliza mabwenyenye hao jinsi walivyopata ardhi hiyo, wao huitiwa polisi.

“Polisi hutukamata mchana na korti yao ni ndani ya magari yao na katika vituo vya polisi lakini hawatufikishi mahakamani,” akasema.

Mzee Said alisema kuwa mabwenyenye hao hudai kuwa wamewatishia maisha.

Alisema huwa wanapokamatwa, polisi huwapiga kichapo cha mbwa hali ambayo imechangia yeye kupata majeraha ya uti wa mgongo.

“Polisi hao huja wawili ama watatu kwa gari lao wakiwa wamejihami kwa bunduki na kutukamata,” akasema.

Kwa sasa, licha ya kuwa anajikaza kutembea, ni lazima ashikiliwe mkono ama aegemee kwa ukuta.

Familia moja kutoka kijiji cha Mwembe Legeza katika wadi ya Shanzu, eneobunge la Kisauni inalilia haki baada ya bwanyenye mmoja kunyakua shamba lao lenye ukubwa wa ekari 21. PICHA | MAUREEN ONGALA

Anatembea akiwa ameinama huku akitetemeka na uso wake ukionyesha dalili ya mtu anayehisi maumivu.

Ingawa alipata matibabu kiasi, lakini hali yake ya kipato duni inafanya kutopata matibabu spesheli anayohitaji. Kwa sababu hii, bado anazidi kustahimili maumivu.

“Kila mara wanakuja na fujo wakitaka kutunyang’anya kipande chetu cha ardhi na kusema wanataka kubomoa nyumba zetu na tukijaribu kuteta wanasema tumewewatishia maisha. Siwezi kutembea kwa sababu polisi waliniumiza mgongo. Mwenzangu tuliyeshikwa naye alipigwa mateke ya mbavu akapata majeraha makubwa na kisha akaaga dunia baadaye. Polisi walikuwa wanatupiga wakisema kuwa sisi ni wajeuri,” akasema.

Familia moja kutoka kijiji cha Mwembe Legeza katika wadi ya Shanzu, eneobunge la Kisauni inalilia haki baada ya bwanyenye mmoja kunyakua shamba lao lenye ukubwa wa ekari 21. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alidai kuwa mabwenyenye hao hutumia maafisa wa polisi kutoka kwa kituo cha polisi cha Bamburi, Kiembeni na Kitengo cha Mbwa almaarufu Dog Section.

“Naishi kwa hofu kwa sababu nikishikwa tena huenda nitaaga dunia kwa sababu hali yangu ya afya sio nzuri kwa sasa. Ninazidi kuwa dhaifu kila siku,” akasema.

Naye Bw Juma Babu alielezea masikitiko yake kuwa polisi wamegeuza magari na vituo vya polisi kuwa ‘mahakama’ ya kuwatetea mabwenyenye wanaowapora wananchi ardhi.

“Sisi tunajua kuwa kesi za mashamba hutatuliwa kortini lakini kwao sivyo. Polisi ndio wamekuwa wakubwa kushughulikia kesi za mashamba kwa kumhangaisha mnyonge,” akasema.

Bw Babu alisema kuwa wamechoka kuhangaishwa na polisi wanaotumiwa na watu hao wanaolenga kuwapora mashamba yao.

“Roho zetu zimechoka kwa sababu ya kuhangaishwa kila siku. Tunataka serikali iingilie kati na kututetea kabla hatujaamua kujitetea,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Cleophas Malala aongoza UDA ‘kulinda’ mali ya...

Raila aagiza maandamano yaishe saa kumi na moja jioni,...

T L