• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Raila aahidi kutunza misitu ya Kaya akishinda urais, kuvumisha Azimio la Umoja katika kaunti zaidi za Pwani

Raila aahidi kutunza misitu ya Kaya akishinda urais, kuvumisha Azimio la Umoja katika kaunti zaidi za Pwani

Na PHILIP MUYANGA

KINARA wa ODM, Raila Odinga ameahidi kwamba, atatunza misitu ya kitamaduni ya Kaya ambayo inaenziwa sana na jamii za Mijikenda na maeneo mengine ya kuabudu nchini akichaguliwa rais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea Jumatano alipokutana na wajumbe wa ODM katika mkahawa wa Diani Reef, kaunti ya Kwale, waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuna haja kubwa ya kuheshimu tamaduni za Kiafrika kwa kuwa “huko ndiko tumetoka.”

“Misitu ya Kaya ni muhimu kwa sababu mababu zetu waliabudu huko,” akasema Bw Odinga ambaye alikuwa akijibu wito wa baadhi ya wazee wa Kaya ambao walimtaka kuhakikisha misitu takatifu inahifadhiwa.

Kiongozi huyo wa ODM aliwaambia wajumbe hao kwamb,a mikutano ya vuguvugu la Azimio la Umoja pia itafanyika katika kaunti za Lamu, Tana River, Kilifi na Taita Taveta.

Bw Odinga jana aliratibiwa kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Upili ya Wasichana Matuga katika kaunti ya Kwale.

Alikuwa ameandamana na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, makatibu wa wizara Hamadi Boga na Safina Kwekwe, miongoni mwa viongozi wengine kutoka eneo hilo.

Bw Odinga alisema kwamba anagombea urais kwa mara ya tano ili kuweka msingi wa utawala bora nchini.

Alisema kwamba hatadumu uongozini kwa muda mrefu bali anachotaka ni kuweka sera za kufaidi vizazi vijavyo.

Kiongozi huyo wa ODM alisema kwamba, anaweza kuimarisha uchumi wa nchi akisikitika kuwa tangu Kenya ilipopata uhuru umasikini haujaangamizwa.

“Nina tajiriba ya kutosha kubadilisha jinsi tunavyofanya mambo. Ninatayarisha manifesto ambayo nitachapisha hivi karibuni,” alisema Bw Odinga.

Waziri mkuu huyo wa zamani alisema kwamba, chini ya utawala wake, kila mtoto atapata nafasi sawa ya elimu katika shule za msingi hadi chuo kikuu na kwamba, ataimarisha afya kwa kuondoa changamoto zinazokabili Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi waahidi kampeni za amani Rift Valley

NDIVYO SIVYO: ‘Nimefika kuchelewa’ ni dhana isiyo na...

T L