• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:41 PM
NDIVYO SIVYO: ‘Nimefika kuchelewa’ ni dhana isiyo na mantiki

NDIVYO SIVYO: ‘Nimefika kuchelewa’ ni dhana isiyo na mantiki

Na ENOCK NYARIKI

BAADHI ya watu wanapokawia kufika mahali walipotarajiwa, hujiwia radhi kwa usemi, ‘Samahani, nimefika kuchelewa.’

Wiki iliyopita tulieleza kwamba usemi huo japo umezoelewa sana katika maongezi, huenda usiwe na mantiki.

Kitenzi {-ja} kinapotumiwa kama kitenzi kisaidizi katika sentensi huibua dhana mbalimbali mojawapo ikiwa nia. Mathalani, kauli ‘amekuja kutufahamisha’inaonyesha lengo la anayezungumziwa ambalo ni kujuza. Dhana nyingine ambayo huibuliwa na kitenzi hicho hasa kinapotumiwa kurejelea wakati ujao ni majuto.

Mfano: Utakuja kulia laiti chanda kingali kinywani. Maana nyingine hujitokeza katika miktadha ya mazungumzo; mingine ambayo ni sahihi na mingine isiyo sahihi. Kwa mfano, mfanyabiashara anapomwambia mteja wake, ‘‘Ukinunua hii bidhaa, utakuja kunikumbuka kauli hiyo huenda isiwe na maana nyingine zaidi ya ushawishi.

Ni muhimu kutaja kuwa si wakati wote ambapo matumizi ya ‘kuja’ katika mawasiliano huleta maana.

Waama yapo maneno mengine licha ya kitenzi chenyewe ambayo hutumiwa tu kama ‘vishikizi’ katika mazungumzo. Mathalani, mtu fulani anaposema ‘wacha nije’ huenda neno ‘wacha’ lisiwe na maana yoyote licha ya kurefusha usemi.

Neno hili likichunguzwa kwa kina, huenda likaonekana kukinzana na linalosemwa yaani ‘wacha’ na ‘nije’ au ‘wacha’ na ‘nimwambie’ katika kauli ‘wacha nimwambie’.

Katika usemi ‘Nimekuja kuchelewa’, kitenzi ‘nimekuja’ hakichangii vyovyote katika kuifanya maana kueleweka. Ukweli ni kuwa kinatatiza maana. Njia rahisi ya kujiwia radhi kwa kuchelewa kufika mahali ni kusema, ‘Samahani, nimechelewa’.

Iwapo ni lazima anayejiradhi atumie maneno mengi, basi aseme, ‘Samahani, nimefika nikiwa nimechelewa.’

You can share this post!

Raila aahidi kutunza misitu ya Kaya akishinda urais,...

Raila adokeza kuhudumu kwa muhula mmoja akishinda urais 2022

T L