• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Raila akaa ngumu kuhusu maandamano 

Raila akaa ngumu kuhusu maandamano 

Na MERCY KOSKEI

KIONGOZI wa Azimio la Umoja Raila Odinga amesisitiza kuwa maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne yataendelea licha ya onyo kali kutoka kwa Kamanda wa Polisi Nairobi.

Hii ni baada ya Mkuu wa Polisi Nairobi Bw Adamson Bungei Jumapili kutangaza kuwa maandamano hayo ni haramu.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Bw Odinga alisema kuwa wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Biashara Moses Kuria.

Hali kadhalika, Waziri Mkuu huyo wa zamani alijumuisha Rais William Ruto kutoa vitisho hivyo.

Hata hivyo, Odinga alishikilia kuwa wataandamana kwa mujibu wa Katiba ya Kenya akisema kuwa kusitisha maandamano hayo ni sawa na kusimamisha Katiba ya nchi.

Raila alisema kuwa Katiba kupitia Kifungu cha 37, inasema kwamba ‘Kila mtu ana haki, kwa amani na bila silaha, kukusanyika, kufanya maandamano na kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka ya umma’ bila kukatazwa.

“Tutatumia haki yetu ya kukusanyika, kuandamana na kuwasilisha maombi yetu siku ya Jumanne kama ilivyotangazwa awali, licha ya vitisho” Odinga alisema.

Kulingana na Bw Odinga waandamanaji watazuru afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuonyesha kuwa kura ziliibiwa na kuagiza uchunguzi wa sava kufanywa na pia kulalamikia kuondolewa kwa makamishna wanne wa tume hiyo.

Odinga pia alisema kuwa watafika katika Afisi ya Rais kufikisha malalamishi ya upinzani, hususan gharama ya juu ya chakula, mafuta na stima.

“Tutatembelea Hazina ya Kitaifa kuomba pesa zote zinazodaiwa na kaunti ziachiliwe mara moja na malipo ya mishahara ya wafanyikazi wote wa umma itolewe muda unaofaa,” taarifa hiyo iliongeza

Odinga alielezea kuwa watazuru Afisi za Utumishi wa Umma, kuwasilisha malalamishi ya jinsi uteuzi wa nyadhifa za serikali unafanywa akisema Kenya ina makabila mengi yanayopaswa kukumbukwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Mmoja aokolewa Shakahola

Wahalifu 4 wa uhalifu watiwa mbaroni

T L