• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Raila alaani uvamizi katika shamba la Uhuru Ruiru

Raila alaani uvamizi katika shamba la Uhuru Ruiru

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa Azimio la Umoja Raila Odinga amekashifu vikali uvamizi katika shamba la familia ya Uhuru Kenyatta eneo la Ruiru mnamo Jumatatu, Machi 27, 2023.

Bw Odinga alisema uvamizi huo ni ishara ya wavamizi wenye nia kunyakua shamba la rais huyo mstaafu.

Wahuni ambao kiongozi huyo wa ODM alidai ni makuhani wa serikali, walivamia Northlands City siku ya maandamano ya Azimio.

Shamba hilo liko katika wadi ya Gatongora, Ruiru, Kaunti ya Kiambu na linaendeleza ufugaji.

Miti ilikatawa katika shamba la Uhuru. PICHA / SAMMY WAWERU

Wavamizi aidha walinaswa kupitia video wakiiba mbuzi na kukata miti kwa kutumia mashine.

Wengine walionekana wakiuza kandokando mwa barabara, na kuingiza kondoo kwenye gari.

Baadhi ya miti iliyokatwa Northlands City ilitumika kuunda makazi ya muda. PICHA / SAMMY WAWERU

Baadhi walijenga makazi ya muda kwa miti na mbao, Raila Odinga akisuta serikali kwa kile alitaja kama kutepetea kulinda mali ya Mkenya.

“Ni aibu kubwa sana wahuni kuvamia shamba la Uhuru Kenyatta, ilhali kuna serikali inayodai imejitolea kulinda mali ya Wakenya,” Odinga akasema, alipozuru shamba hilo mnamo Jumanne.

Kiongozi wa Azimio la Umoja Bw Raila Odinga akizungumza katika shamba la Uhuru Kenyatta, Northlands City, lililovamiwa Jumatatu, Machi 27, 2023. PICHA / SAMMY WAWERU

Akilaani tukio hilo, kiongozi huyo wa upinzani alihusisha Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na mwenzake wa Kiharu, Ndindi Nyoro kwa uvamizi huo.

Alidai kwamba viongozi hao wa Kenya Kwanza ndio walihusika na njama ya kuvamia na kuharibu mali ya Uhuru.

“Wamekuwa wakisema wao ni watoto wa MauMau, na matamshi yao ya hivi karibuni yanaashiria wanahusishwa na tukio la aibu kuvamia shamba la Kenyatta,” alihoji.

Shamba la Northlands City lilichomwa jioni ya Jumatatu, Machi 27, 2023. PICHA / SAMMY WAWERU

Hata ingawa idara ya polisi kupitia Inspekta Jenerali Mkuu, IG Japhet Koome imetangaza kuanzisha uchunguzi wa uvamizi huo, Bw Raila alielezea kushangazwa kwake na hatua ya polisi kutoitika tukio hilo lilipokuwa likiendelea.

“Inspekta Jenerali ameongea kulihusu ila anadai polisi hawakujua likitokea. Wanafikiria Kenya ina upungufu wa wajinga, tunasema ole wao,” alihoji.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, Mabw Kalonzo Musyoka (Wiper), George Wajackoyah wa Roots Party, aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni, aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Euegene Wamalwa, wote wakikashifu uvamizi wa shamba la Uhuru.

Chupa ya maji iliyoachwa na waliovamia shamba la Northlands City. PICHA / SAMMY WAWERU

Kufuatia uvamizi wa Jumatatu, walioshiriki kando na kudai kujigawia ardhi, walionyesha cheti cha kumiliki vipande vya ploti walizojinyakulia.

Bw Ichungwa hata hivyo amejitokeza akijitetea kwamba hakuhusishwa na uvamizi wa Northlands City.

Jumatatu jioni, moto mkubwa uliteketeza sehemu ya shamba hilo.

  • Tags

You can share this post!

Raila aongeza kasi ya maandamano jijini

Papa Francis aendelea kupata nafuu baada ya kulazwa

T L