• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Ruto alikerwa na Raila – Wandani

Ruto alikerwa na Raila – Wandani

Na IBRAHIM ORUKO

NAIBU Rais William Ruto alikwepa kongamano la ugatuzi katika Kaunti ya Makueni Ijumaa wiki jana, kwa kukerwa na hadhi ambayo waandalizi walimpa kiongozi wa ODM, Raila Odinga wakati wa ufunguzi wake.

Dkt Ruto alikuwa ameratibiwa kuongoza hafla ya kufungwa kwa kongamano hilo, lakini akafeli kufika dakika za mwisho.

Sasa imeibuka kuwa uamuzi huo ulikuwa wa kimakusudi na uliolenga hatua ya Baraza la Magavana (CoG) ya kumwalika Bw Odinga kuongoza hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo.

Baadhi ya wabunge wa mrengo wa Tangatanga waliambia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto aliamua kutofika Makueni baada ya kung’amua kuwa CoG iligeuza kongamano kuwa kama jukwaa la kupigia debe azma ya urais ya Bw Odinga.

Kando na kuhutubia kongamano hilo siku ambayo Rais Kenyatta alilifungua rasmi, Bw Odinga alisindikizwa hadi Makueni na mawaziri sita, akiwemo Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA), ambacho Dkt Ruto anatarajiwa kutumia kuwania urais, kilihusisha hatua ya mawaziri hao na uchaguzi wa urais 2022.

“Naibu Rais hatarajiwi kuongoza hafla ya kufunga kongamano ambalo lilifunguliwa na kiongozi wa upinzani,” akasema mbunge mmoja anayeegemea chama cha UDA.

Kando na kutofika katika kongamano hilo, hakutuma ujumbe wa pole kwa waandalizi.Sekritariati ya CoG ilipompigia simu Dkt Ruto, Alhamisi ili athibitishe kuwa atahudhuria, aliahidi kumtuma mkuu wa wafanyakazi afisini mwake, Bw Ken Osinde amwakilishe.

Magavana walimkataa afisa huyo.

Hatimaye, shughuli ya kufunga kongamano hilo, iliendeshwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, ambaye alialikwa dakika za mwisho na akakubali.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, alisema kuwa hilo lilikuwa kongamano la hadhi ya kimataifa na halikupaswa kufungwa na afisa wa hadhi ya Bw Osinde.

Ratiba iliyotolewa siku chache kabla ya kuanza kwa kongamano hilo, ilionyesha kuwa Rais Kenyatta angeongoza hafla ya ufunguzi.

Bw Odinga angetoa hotuba rasmi siku ya pili huku Dkt Ruto akiongoza hafla ya kulifunga, jinsi ambavyo viongozi hao watatu wamekuwa wakifanya katika makongamano ya sita yaliyofanyika miaka ya nyuma.

Lakini ratiba ya mwaka huu ilifanyiwa mabadiliko dakika za mwisho, ambapo Bw Odinga aliorodheshwa kulihutubia siku ya kwanza pamoja na Rais Kenyatta.

Jaji Mkuu Martha Koome alihutubu siku ya pili ambapo aliwashutumu wandani wa Dkt Ruto akiwaambia kuwa hatajiuzulu kutoka kamati inayoongoza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Utata uligubika kongamano hilo baada ya Rais Kenyatta kuelekea Afrika Kusini kwa ziara rasmi wakati ambapo alitarajiwa kuongoza hafla ya ufunguzi.

Hali hiyo iliibua uvumi ambao ulikasirisha wandani wa Dkt Ruto, akiwemo Waziri wa Ugatuzi Charles Keter, ambao waliondoka baada ya hotuba ya Rais Kenyatta aliyotoa kwa njia ya mtandao kutoka Afrika Kusini.

Uvumi wenyewe ulikuwa ni kwamba Bw Odinga ndiye angetwikwa jukumu la kusoma hotuba ya kiongozi wa taifa.

Baadaye, afisa mmoja kutoka afisi ya Rais alimpigia simu mwenyekiti wa CoG Martin Wambora, akimweleza kuwa Waziri Matiang’i ndiye angemwakilisha Rais Kenyatta kwa kusoma hotuba yake rasmi.

Baadaye, taarifa nyingine ilienezwa kwamba Bw Odinga na Dkt Matiang’i wangemwakilisha Rais Kenyatta.Taarifa hizo zilimkasirisha Bw Keter ambaye ilionekana kwamba hakuwa na ufahamu wowote kuhusu suala hilo.

Mawaziri wengine waliokuwa katika ujumbe wa Bw Odinga ni; Monica Juma (Kawi), Bw Wamalwa (Ulinzi), Joe Mucheru (ICT) na Keriako Tobiko (Mazingira na Mali Asili).

Waziri Keter alipigwa na mshangao Dkt Matiang’i alipotangaza dakika za mwisho kwamba Rais Kenyatta angewasilisha hotuba yake kupitia video kutoka Afrika Kusini.

Baada ya hapo Bw Keter aliondoka kabla ya Bw Odinga na ujumbe wake pia kuondoka jukwaani.

You can share this post!

Omariba, Sakawa mabingwa vishale Makavazi Cup

STEVE ITELA: Hatua ya jeshi kusimamia mashirika isiwe fursa...

T L