• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
STEVE ITELA: Hatua ya jeshi kusimamia mashirika isiwe fursa ya KDF kutwaa ardhi isiyo yake

STEVE ITELA: Hatua ya jeshi kusimamia mashirika isiwe fursa ya KDF kutwaa ardhi isiyo yake

Na STEVE ITELA

SERIKALI ya Jubilee imekuwa ikiweka mashirika mbalimbali ya serikali ambayo yanaelekea kuporomoka au yanakabiliwa na changamoto kadhaa za kifedha chini ya usimamizi wa Jeshi la Nchi (KDF).

Kiwanda cha Nyama (KMC) ni kati ya mashirika ya serikali ambayo usimamizi wake ulitwaliwa na KDF hivi majuzi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuru hivyo.

Chama cha Mawakili nchini (LSK) kilielekea kortini na kupinga hatua hiyo.

Japo korti iliamua kuwa hatua ya Rais Kenyatta ilikuwa kinyume cha sheria, kwa kuwa hitaji la kisheria la kupokea maoni ya raia lilipuuzwa wakati wa mchakato huo, KDF bado inaendelea kusimamia kiwanda hicho na hata imetekeleza mageuzi makubwa.

Hasa serikali ililenga kuhakikisha kuwa usimamizi duni wa KMC unatokomezwa hadi shirika hilo likaanza kupata faida kisha kubuni nafasi kadhaa za ajira.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi wanaona hatua ya KDF kutwaa usimamizi wa KMC kama mwenendo unaoibuka wa serikali kuyaweka mashirika mbalimbali chini ya usimamizi wa jeshi.

Hata hivyo, suala tata ambalo limekuwa likichipuka ni kuhusu umiliki wa ardhi za KMC baada ya KDF kutwaa usimamizi wake.

Aidha, jamii ambazo zina ardhi karibu na mashirika hayo nazo zimekumbwa na wasiwasi kuwa ardhi zao zitatwaliwa au kutumiwa kama sehemu ya wanajeshi kufanyia mazoezi au kujengwa kwa kambi za kijeshi.

Mnamo 2020, madiwani wa Kaunti ya Taita Taveta, ambayo imekumbwa na dhuluma za kihistoria kuhusu ardhi na hivyo kuwa na maskwota wengi, walipinga vikali kugeuzwa kwa ranchi sita kuwa ardhi ya kijamii.

Diwani wa Wadi ya Kasigau alipinga vikali kugeuzwa kwa ranchi hizo; Mramba, Development Trust, Ndara B, Oza, Mbulia, Kishamba na Teri B ambazo mwanzoni hazikuwepo katika sajili ya ardhi kama ya kijamii.

Hatua hiyo iliibua maswali kuhusu ukiukaji wa sheria kuhusu umiliki wa ardhi katika kaunti hiyo. ya Pwani mwa nchi.

Isitoshe, KDF baadaye ilidai ekari nyingine 24,000 za ardhi ya ranchi kujenga kambi ya mazoezi ya jeshi kwenye wadi ya Kasigau.

Ingawa iliandaa mkutano na wamiliki wa ranchi hizo, ilishangaza kuwa KDF ilitaka ardhi hiyo ilhali ina ekari kadhaa za ardhi ambazo tayari imejengea kituo cha jeshi.

Vilevile, imeshatwaa ranchi ya Taita na ekari nyingine 3,000 za ardhi kwenye lokesheni ya Kuranze na Kasigau.

Je ilitakia ardhi nyingine kwa nini?

Ni vyema serikali ifahamu kuwa Kaunti ya Taita Taveta pia ina ardhi ambayo ni sehemu za mbuga ya wanyamapori hasa Ndovu. Kwa hivyo, KDF haifai kupokezwa ardhi zaidi kujenga kambi ya kijeshi.

Aidha kuna kesi ambazo zimepelekwa mahakamani na hata Tume ya Ardhi Nchini (NLC) imeshtakiwa.

Ni vyema serikali isubiri kesi hizo ziamuliwe badala ya kupigania kutwaa vipande kadhaa vya ardhi.

KDF isiruhusiwe tu kutwaa ardhi za wenyewe eti kwa sababu imechukua usimamizi wa mashirika ya serikali.

  • Tags

You can share this post!

Ruto alikerwa na Raila – Wandani

Kagwe awaharibia Wakenya Krismasi

T L