• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ruto hatimaye akubali Mswada urekebishwe

Ruto hatimaye akubali Mswada urekebishwe

NA WAANDISHI WETU

RAIS William Ruto amesalimu amri na kukubali kupunguza ushuru wa mafuta na makato ya mradi wa nyumba nafuu kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi.

Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango sasa imependekeza kupunguzwa kwa makato ya nyumba nafuu kutoka asilimia 3 hadi asilimia 1.5.

Mswada wa Fedha wa 2023 ulipendekeza kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa mbalimbali ili kuwezesha Rais Ruto kupata fedha za kutosha kufadhili bajeti yake ya kwanza ya Sh3.6 trilioni.

Wabunge ambao ni wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Molo, Kuria Kimani, walisema kuwa ushuru wa mafuta utasalia asilimia 8.

Mswada huo ulipendekeza kuongezwa kwa ushuru wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.

Pendekezo la kuongeza ushuru huo lilipingwa vikali na Wakenya huku wataalamu wakisema ungesababisha kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu kama vile chakula.

Watengenezaji wa video za mtandaoni pia wamepata afueni baada ya kamati hiyo kupendekeza wapunguziwe ushuru kutoka asilimia 15 hadi asilimia 5.

Kamati hiyo iliyokuwa ikitathmini mswada huo mjini Naivasha, Nakuru, inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake Bungeni leo mchana.

Awali, Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walikuwa wameshikilia kuwa ni sharti mswada huo upitishwe jinsi ulivyo. Lakini Wakenya waliupinga mswada huo kupitia vyombo vya habari huku wengine wakienda kortini kujaribu kushinikiza wizara ya Fedha kuutupilia mbali.

Zaidi ya Wakenya 1,000 walipeleka pingamizi zao kwa njia ya maandishi Bungeni.

Hata hivyo, kamati hiyo imeacha mlango wazi kwa wabunge kurekebisha baadhi ya vifungu vya mswada huo ambavyo watahisi huenda vikafinya raia.

Miongoni mwa mapendekezo ambayo kamati hiyo imeachia wabunge wenzao Bungeni ni kupandishwa kwa ushuru wa malipo ya unga wa mahindi, sementi kutoka ng’ambo, vipodozi na juakali.

Iwapo wabunge wataidhinisha ripoti ya kamati hiyo bila kuifanyia marekebisho, Wakenya wanaopata mshahara wa Sh500,000 na zaidi watakuwa kati ya raia watakaohisi uchungu kwani watatozwa ushuru wa asilimia 35 huku wenzao wa mishahara ya chini wakikatwa asilimia 30.

Wanachama watatu wa kamati hiyo waliozungumza bila kutaka kutajwa majina jana Jumapili waliiambia Taifa Leo kwamba wamepata kibali cha Rais Ruto kutekeleza mabadiliko hayo.

“Hata tunapomaliza kuandika ripoti itakayowasilishwa katika Bunge, tuna idhini ya Rais kupendekeza mageuzi yatakayogusia malalamishi ya Wakenya kabla ya mswada huo kupitishwa na Bunge,” mbunge mmoja akafichua.

Kuanzishwa kwa ushuru wa nyumba kumezua malalamishi ya raia, huku suala la gharama ya juu ya maisha likiendelea kuzua mdahalo mkali nchini.

Kipengele kinachopendekeza ushuru wa asilimia 30 kwa fedha zinazolipwa maafisa walio kazini hakikupendekezwa kufanyiwa mageuzi na kamati hiyo.

Hilo linazua maswali kuhusu vile maafisa hao watakavyokidhi mahitaji yao, kwani marupurupu si kipato, bali usaidizi maalum wa kifedha kumwezesha mfanyakazi kugharimia mahitaji ya kimsingi.

Suala jingine ambalo litazua ghadhabu za Wakenya dhidi ya kamati hiyo ni pendekezo la kubadilisha kiwango cha vyakula vya kawaida kama unga wa mahindi, unga wa mhogo na vyakula vingine kutoka bidhaa za kutotozwa ushuru hadi bidhaa za kawaida zinazofaa kutozwa ushuru.

Hilo linamaanisha kuwa gharama yake itapanda, hivyo basi kuongeza gharama ya maisha. Mswada huo pia unalenga kubadilisha hali ya bidhaa kama dawa za matibabu, dawa za kilimo na mbolea, na usafirishaji wa miwa kutoka mashambani hadi viwandani kutoka sufuri hadi kiwango cha kutotozwa ushuru.

Hilo bila shaka linaongeza gharama za dawa za matibabu, gharama ya matibabu na chakula, ikiwemo sukari iliyozalishiwa humu nchini.

Hilo linakinzana na ahadi ya serikali ya Kenya Kwanza ya kupunguza gharama ya uzalishaji. Utawala wa Kenya Kwanza pia unataka kuongeza ushuru wa saruji iliyoagizwa kutoka nje.

Ripoti za Vitalis Kimutai, Macharia Mwangi na David Mwere

  • Tags

You can share this post!

Gachagua ahofia maisha yake akidai makateli wa kahawa si...

Seahorses Aquatic Center yatawala mashindano ya kuogelea ya...

T L