• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Seahorses Aquatic Center yatawala mashindano ya kuogelea ya Kiambu

Seahorses Aquatic Center yatawala mashindano ya kuogelea ya Kiambu

Na GEOFFREY ANENE

MELISSA Alala na Dayo Mbugua waliongoza timu ya Seashorses Aquatic Center kutawala mashindano ya kuogelea ya Shirikisho la Uogeleaji Kenya (KSF) tawi la Kiambu katika shule ya kimataifa ya Crawford katika eneo la Tatu City, Kiambu, Jumamosi.

Alala alishinda vitengo sita vya waogeleaji walio na umri wa kati ya miaka minane hadi tisa, huku Seahorses ikimaliza ya kwanza kwa kuzoa jumla ya pointi 321.

Ilifuatiwa na Water Warriors Swim Club (pointi 119), Woodcreek School (86), Crawford International School (65) na Aqua Warriors (45) katika orodha ya timu tano-bora za wasichana, mtawalia

Mbugua alivuna mataji manne katika kitengo chake cha umri wa miaka saba katika mashindano ya wavulana ambayo Seashorses ilivuna jumla ya pointi 382 ikifuatiwa na Montessori Learning Center na Woodcreek (59 kila mmoja) kwenye mashindano hayo ya siku moja.

Wenyeji Crawford waliridhika na nafasi ya nne kwa alama 54 wakifuatiwa na Otters Swim Club (25), Kiota School (18), Aqua Warriors (16), Riara International School (14), Lustars Swim Club (12) na Oshwald Academy Nairobi (nne).

Mbali na Alala, Seahorses pia walibeba mataji ya kibinafsi kupitia kwa Kaari Ngugi (umri wa miaka saba 100 SC Individual Medley & 50 SC Meter Breaststroke), Abigail Wanjugu (miaka saba 50 SC Meter Backstroke), Njeri Ng’ang’a (miaka sita 25 SC Meter Butterfly), Bristol Maina (miaka mitano na chini 25 SC Meter Backstroke), Amarachi Wangui (miaka sita 25 SC Meter Backstroke) na Naya Olengo (miaka saba 25 SC Meter Backstroke).

Washindi wengine wa Seahorses katika vitengo vya wavulana ni Nathan Ngugi (umri wa 8-9 100 SC Meter IM & 50 SC Meter Butterfly), Ethan Innocent (8-9 100 SC Meter IM, 50 SC Meter Breaststroke & 50 SC Meter Breaststroke), Zion Kelly (miaka sita 25 SC Meter Butterfly), Kago Inzoberi (miaka saba 25 SC Meter Butterfly & 50 SC Meter Breaststroke), Fadhili Osunga (miaka 8-9 25 SC Meter Butterfly), Daniel Mathenge (miaka mitano na chini 25 SC Meter Backstroke) na Liam Kariuki (umri wa 8-9 25 SC Meter Backstroke).

Jacqueline Macharia, ambaye ni naibu katibu wa KSF-Kiambu, alisema kuwa mashindao hayo yalikuwa muhimu kwa sababu ni ya kufunga msimu 2022-2023.

“Baada ya mashindano haya, tunaenda likizo hadi Agosti, ingawa mazoezi yataendelea,” alisema Macharia almaarufu Coach Jackie.

Katika mashindano ya Jumamosi, KSF-Kiambu ilishirikiana na shule ya kimataifa ya Crawford iliyotoa bwawa lake.

“Ni bwawa la mita 25. Inafurahisha kuona watoto wakiogelea wakati wowote iwe ni wakati wa mvua ama jua. Wanapofundishwa wakiwa wadogo wanapata kuondoa uoga wa maji na wanapokuwa wanaweza kuogelea kwa usalama,” alieleza.

Coach Jackie anatumai kuwa mafunzo na mashindano ya kuogelea yatasaidia katika kupunguza visa vya watu kufa maji katika kaunti ya Kiambu.

“Kuna visa vingi sana vya watu kufa maji Kiambu,” alidokeza.

KSF-Kiambu pia inajitahidi kushawishi shule za umma na jamii zisizojiweza kifedha kujiingiza katika mchezo wa uogeleaji na kuukumbatia. Katika makala haya, KSF-Kiambu ilichagua kudhamini shule ya msingi ya umma ya Mugumo-Ini kutoka mitaa ya mabanda ya Kiandutu mjini Thika.

“Mugumo-Ini iliwasilisha waogeleaji 14. Tuliamua kuwasaidia kwa sababu ni jukumu letu kuinua mchezo wa kuogelea. Tutaendelea kusaidia shule za umma kutoka jamii zisizojiweza hapa Kiambu kushiriki mashindano kila mara,” alitangaza kocha huyo.

KSF-Kiambu pia imenunua vifaa vya kupima kasi ya waogeleaji ili kuimarisha kunakili muda ya watoto katika mashindano kuanzia msimu ujao.

Kocha wa klabu ya kuogelea ya Hydrofit, Gideon Malova alishukuru waogeleaji kutoka kaunti za Kiambu, Nairobi na Murang’a kwa kujitokeza katika mashindano hayo bila ya kusahau makocha, wazazi na mashabiki.

“Hatuzuii washiriki kutoka umri fulani katika juhudi za kukuza wanaolimpiki wa siku za usoni,” alisema Coach Jackie.

  • Tags

You can share this post!

Ruto hatimaye akubali Mswada urekebishwe

Turathi na vivutio vya kipekee vya Lamu

T L