• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Askofu Ole Sapit asimama imara kuzima siasa kanisani

Askofu Ole Sapit asimama imara kuzima siasa kanisani

Na MAUREEN ONGALA

WANASIASA waliohudhuria ibada ya kumtawaza askofu mpya wa Kanisa la Anglikana (ACK) atakayesimamia jimbo la Malindi, walilazimika kutulia tuli sawa na waumini wengine baada ya kunyimwa nafasi ya kuhutubu maabadini.

Askofu Mkuu wa ACK nchini, Jackson Ole Sapit, alisisistiza kwamba hakuna siasa itakayopigwa katika ibada na sherehe za kuabudu katika kanisa hilo.

Kulinganga na Sapit, wanasiasa wana uhuru wa kutangamana na kupiga siasa nje ya kanisa baada ya ibada za kanisa hilo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanywa katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi mnamo Jumapili, Bw Sapit aliwataka wanasiasa kutofautisha ibada na mikutano ya siasa.

“Hatutawapa nafasi ya kuongea, labda wakati wa maankuli. Tukisema tutofautishe sherehe za ibada na nyinginezo sio kuwa hatuwapendi,” akasema.

Askofu Reuben Katite anachukua nafasi ya askofu mstaafu, Dkt Lawrence Dena.

Baadhi ya wanasiasa kutoka Kaunti ya Kilifi akiwemo Gavana Amason Kingi walihudhuria sherehe hiyo.Wengine waliokuwepo ni Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, Wabunge Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Teddy Mwambire (Ganze), Bi Aisha Jumwa (Malindi), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo, Bi Gertrude Mbeyu na Naibu Gavana Gideon Saburi.

Wanasiasa hao hawakutambulika kila walipokuwa wanaingia kama ilivyo desturi katika sherehe nyingine.

Walitakiwa kuingia kwa unyenyekevu na kila mtu kutafuta kiti chake.

Hata hivyo Bi Jumwa aliwapa salamu akina mama alipokuwa akiingia, hali ambayo ilizua gumzo kwa muda mfupi.

Hali ya kawaida ilirejea baada ya Bw Sapit kuwatuliza na kuwaomba kuendelea na ibada.

Bw Sapit aliwatambua viongozi hao baada ya sherehe kukamilika na waliruhisiwa kumpa salamu za heri Askofu Katite.

Ibada ilipokuwa inakaribia kuisha wengine wao walianza kujitayarisha kuondoka kwa haraka.

Askofu Katite aliye na umri wa miaka 42, anatarajiwa kuhudumu katika wadhifa wake kwa miaka 23 hadi atakapostaafu.

Baadhi ya waumini walipendekeza sheria za uongozi wa kanisa zibadilishwe ili Askofu awe akitumikia jimbo kwa miaka mitano au saba pekee na kuwapa wengine nafasi.

You can share this post!

Messi aweka rekodi ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or...

Mtihani kwa Uhuru kipindi cha lala salama

T L