• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Sapoti ya Wakenya iko juu, mamake Jeff Mwathi asema akiomba walio na fununu kuhusu kifo cha kijana huyo wajitokeze

Sapoti ya Wakenya iko juu, mamake Jeff Mwathi asema akiomba walio na fununu kuhusu kifo cha kijana huyo wajitokeze

NA RICHARD MUNGUTI

MAMA yake msanii Jeff Mwathi aliyeaga dunia katika makazi ya DJ Faxto amemrai yeyote aliye na ushahidi wowote wa jinsi mwanawe alivyoangamia ajitokeze ndipo haki itendeke.

“Namsihi yeyote aliye na ushahidi wa jinsi mwanangu alivyofariki ajitokeze na kuupeana kwa polisi au kwa wakili wa familia Danstan Omari ili haki itendeke,” Bi Anne Mwathi alisema Alhamisi akizungumza na wanahabari katika mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi.

Bi Mwathi alieleza kwa masikitiko makubwa jinsi mwanawe alivyouawa na kuzikwa na kufukuliwa tena kufanyiwa upasuaji mara nyingine na mtaalam wa Serikali Dkt Johansen Oduor.

“Kulia nimelia. Machozi yamekauka mwilini na sasa naomba haki itendeke,” Bi Mwathi ameeleza wanahabari.

Mama huyo mwenye watoto wawili aliomba serikali isisite kumchukulia hatua aliyemuua mwanawe “hata kama ni nani.”

Akasema, “Anayefanya makosa lazima aadhibiwe kwa mujibu wa sheria hata kama ni nani.”

Mama huyo aliwapongeza wote waliompigia simu kumliwaza.

Kilio cha Mama Jeff kiliungwa mkono na wakili Danstan Omari aliyetoa wito kwa yeyote aliye na habari kuhusu kuuawa kwa Jeff afike katika afisi zake.

“Yeyote anayeogopa kuuawa kwa kufichua ukweli afike katika afisi yangu kuandikisha taarifa. Nitahakikisha usalama wake upo pamoja na kurai asasi ya serikali inayohusika na kuweka usiri wa mashahidi kuwahifadhi,” Omari alisema.

Bi Mwathi na Bw Omari walisema hayo baada ya mahakama ya Milimani kutenga uchunguzi kuanza Agosti 10, 2023.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameorodhesha mashahidi 35.

Akitenga siku ya kuanza kupokea ushahidi, hakimu mwandamizi Zainab Abdul alisema mauaji ya kinyama ya Mwathi yaliwashtua wengi huku maelfu ya watu wakipigwa na butwaa.

Mwathi aliyekuwa mwanafunzi katika chuo cha Nairobi Institute of Business Studies (NIBS), aliaga dunia katika makazi ya DJ Fatxo mnamo Februari 22, 2023.

Marehemu Jeff Mwathi. PICHA | MAKTABA

Mwathi alikufa katika mazingira tata na hata kuzikwa kwake kuliibua hisia tele katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru.

Alizikwa kisha akafukuliwa tena mwili wake kufanyiwa upasuaji tena.

Hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Bw Omari alisema atahakikisha kwamba haki imetendeka katika uchunguzi huo wa mahakama.

Wakili huyo aliyejitolea kuwakilisha familia ya Jeff bila malipo alisema inasikitisha Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) alishindwa kuwatia nguvuni waliomuua mwanafunzi huyo wa chuo cha NIBS.

Bw Omari alisema yuko na uhakika haki itatendeka na kwamba “hatachoka hadi haki itendeke katika mauaji ya kinyama ya Jeff Mwathi.”

Bw Omari alisema ataelezea ulimwengu ukweli utakaochipuka katika uchunguzi huo wa mauaji ya kijana Mwathi.

  • Tags

You can share this post!

Gor, Tusker na Homeboyz taabani kwa kukosa timu za wanawake

Awali ilikuwa milio ya risasi na magaidi Lamu, sasa ni...

T L