• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Seneti yashangazwa na idadi kubwa ya makaimu serikalini

Seneti yashangazwa na idadi kubwa ya makaimu serikalini

NA MARY WANGARI

TUME ya Kuajiri Wafanyakazi wa Umma (PSC) imemulikwa kuhusiana na idadi kubwa ya wafanyakazi wa umma katika asasi na wizara za serikali wanaohudumu katika nyadhifa zao wakiwa makaimu.

Hii ni baada ya kubainika kuwa karibu wanachama wote wa Bodi ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) akiwemo Kamishna Mkuu Rispah Simiyu, wanahudumu kama makaimu.

Mwenyekiti wa Bodi ya KRA, Anthony Mwaura, ndiye pekee aliye na wadhifa rasmi katika Mamlaka hiyo, Seneti ilielezwa katika kikao mnamo Jumanne.

Kamati ya Seneti kuhusu Uwiano imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa maafisa wa umma wanaoshikilia nyadhifa muhimu kwa muda mrefu kama makaimu bila kuajiriwa rasmi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Marsabit, Mohamed Chute kama mwenyekiti, imezua maswali kuhusu ni kwa nini asasi za serikali zinazidi kuwa na idadi kubwa ya maafisa ambao bado hawajaajiriwa rasmi licha ya kushikilia nyadhifa kuu

Wakiongozwa na Seneta wa Uasin Gishu, Jackson Mandago, walionya kwamba mtindo wa kuweka maafisa wa umma kama makaimu miaka nenda miaka rudi bila kuwaajiri huenda ndio unalemaza na kusababisha utoaji huduma kudorora katika asasi mbalimbali za serikali.

“Ni kana kwamba kuna wadhifa unaoitwa kaimu katika asasi za serikali. Kumekuwa na ongezeko la watu wanaohudumu kama makaimu kwa hadi miaka mitatu. Mbona wasithibitishwe na kuajiriwa rasmi?” alihoji Seneta Mandago.

Kulingana na Seneta Chute, “Mwenyekiti wa Bodi ya KRA huenda ndiye pekee anayeshikilia wadhifa uliothibitishwa rasmi.”

Kamati hiyo imealika uongozi wa KRA wakiwemo Mwenyekiti na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw Mwaura na Bi Simiyu mtawalia, kujiwasilisha binafsi mnamo Alhamisi wiki ijayo.

Aidha, KRA imetakiwa kuwasilisha orodha ya watu walioajiriwa na nyadhifa zao katika shughuli iliyokamilika majuzi kwa lengo la kutathmini ujumuishaji kimaeneo, kijinsia na watu wanaoishi na ulemavu.

Haya yalijiri baada ya Bi Simiyu kususia kikao cha kamati hiyo kwa mara ya pili ambapo alialikwa kujadili ujumuishaji wa wanaoishi na ulemavu na mchakato huo wa ajira kwa ujumla.

“Tumemwalika Kamishna Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya KRA kujiwasilisha binafsi Alhamisi wiki ijayo la sivyo tutatoa amri ya kuwashurutisha kuja,” alisema seneta Chute.

“Suala la ujumuishaji wa watu wanaoishi na ulemavu katika asasi za umma ni jambo muhimu kitaifa. Tunataka pia orodha ya maelfu ya maafisa walioajiriwa ili tujue ni wangapi wameajiriwa rasmi, wangapi ni wanawake, suala la ujumuishaji kijinsia na walemavu.”

Seneti vilevile imewamulika maafisa wakuu katika taasisi za umma wanaosusia mialiko ya Kamati za waundasheria kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayohusu mashirika wanaoyosimamia.

“Ni sharti kuwe na utaratibu katika utumishi wa umma. Hatuwezi kuwa tukituma barua kila mara kwa wanaosimamia idara mbalimbali kisha wanapuuza bila sababu thabiti,” alihoji Seneta Maalum Raphael Chimera.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala atua mjini Monaco kuwinda ushindi katika Diamond...

Tuokoe nchi yetu

T L