• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Serikali ya Kenya Kwanza yapunguza pesa za wazee

Serikali ya Kenya Kwanza yapunguza pesa za wazee

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imepunguza kwa kiasi kikubwa mgao wa fedha za kuwafaa wakogwe, mayatima, watu wanaoishi na ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum, kwa kima cha Sh1.3 bilioni, kulingana na Bajeti ya Mwaka wa Kifedha wa 2023/2024.

Akiongea Alhamisi alipowasilisha bajeti hiyo ya kwanza chini ya utawala wa Kenya Kwanza, Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u alisema kuwa serikali imetenga Sh38.2 bilioni za malipo ya watu hao.

Hii ni tofauti na Sh39.5 bilioni zilizotengewa makundi hayo ya Wakenya katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023 unaofika tamati mnamo Juni 30, 2023.

“Kutokana na mgao huo wa bajeti, Sh18 bilioni zitagharimia malipo ya wazee, nao mayatima wametengewa Sh7.9 bilioni huku watu wanaoishi na ulemavu (PLWDs) wakitengewa Sh1.2 bilioni,” Profesa Ndung’u akasema.

Chini ya mpango huo unaojulikana kama Inua Jamii, wanaofaidi hulipwa Sh2,000 kila mwezi za kuwasaidia kugharimia mahitaji yao ya kimsingi.

Lakini tangu Rais William Ruto alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022 makundi hayo yamepokea malipo yao mara moja pekee, mnamo Januari 9, 2023.

Walipokea malimbikizo ya malipo ya miezi minne tangu Julai 2022 hadi Oktoba 2022, ambapo kila mmoja wao alilipwa Sh8,000.

Mnamo Alhamisi, Waziri Profesa Ndung’u alisema kuwa kuanzia Julai 1, 2023 watu hawa watakuwa wakilipwa kwa wakati, sawa na watumishi wa serikali.

  • Tags

You can share this post!

Utajuaje familia yenye mshikamano na ushirikiano mzuri?

Siku ya Mtoto wa Kiafrika: Mashirika ya haki za binadamu...

T L