• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Wafanyakazi kuanza kukatwa ushuru wa nyumba

Wafanyakazi kuanza kukatwa ushuru wa nyumba

NA CHARLES WASONGA

MISHAHARA ya wafanyakazi itapungua kwa kima cha asilimia 1.5 kuanzia mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti serikali itakapoanza kukusanya ushuru wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Hii ni kufuatia hatua ya Mahakama ya Rufaa wiki jana kuruhusu utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023 hadi kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu na Seneta wa Busia Okiya Omtatah itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mahakama hiyo iliweka kando amri iliyotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Mugure Thande ya kusitisha utekelezaji wa sheria hiyo iliyopingwa na Wakenya wengi.

Kupitia notisi iliyowekwa magazetini Alhamisi, Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji itaanza kutoza ushuru huo wa nyumba kuanzia Julai 1, 2023.

“Ushuru huo utalipwa na wafanyakazi kwa kiwango cha asilimia 1.5 ya mishahara yao kila mwezi. Waajiri nao watalipa ushuru wa kiwango sawa na hicho kwa wafanyakazi wao kila mwezi,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Charles Hinga.

“Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji imeteua Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) kama ajenti wa kukusanya ushuru huo. KRA itatoa taarifa kushauri wahusika kuhusu mbinu ya ukusanyaji wa ushuru huu,” Bw Hinga akaongeza.

Hii ina maana kuwa mfanyakazi anayepokea mshahara wa chini wa Sh20,000 kwa mwezi atatozwa ushuru wa Sh300 kila mwezi, pesa zitakazohifadhiwa katika Hazina ya Nyumba.

Naye mfanyakazi anayepokea mshahara wa Sh50,000 atapoteza Sh1,500 mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti huku wale wanaopokea Sh500,000 wakikatwa Sh7,500 zaidi kama ushuru wa nyumba.

Kulingana na Sheria hiyo ya fedha ilipingwa vikali na upinzani na vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi, mwajiri anayefeli kuwasilisha ushuru wa nyumba kwa KRA atatozwa faini ambayo ni sawa na asilimia mbili pesa ambazo alifeli kuwasilisha kwa mamlaka hiyo kila mwezi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya sarakasi

Ulawiti: Papa Francis asema viongozi wa kidini wahitaji...

T L