• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Serikali yaagiza masomo kurejelewa Nairobi, Mombasa na Kisumu

Serikali yaagiza masomo kurejelewa Nairobi, Mombasa na Kisumu

NA CHARLES WASONGA

WIZARA za Elimu na Usalama wa Ndani Jumatano jioni zimetangaza kufunguliwa kwa shule za kutwa katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Kisumu ambazo zilikuwa zimefungwa baada ya kile kilichotajwa kama “kuimarika kwa usalama”.

Wizara hizo Jumanne zilikuwa zimeagiza shule kufungwa kutokana na hofu ya utovu wa usalama kufuatia maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya kushinikiza serikali ipunguze gharama ya maisha na kupunguza ushuru.

“Sasa serikali imetathmini hali ya usalama katika sehemu mbalimbali nchini na sasa inaridhika kuwa utulivu umerejea maeneo mbalimbali nchini, zikiwemo kaunti za Nairobi, Mombasa na Kisumu. Maafisa wa usalama wameridhika kuwa hali ya usalama imeimarika katika kaunti hizi tatu na maeneo mengine nchini. Kwa msingi huu, inaamuriwa kwamba shule zote za kutwa katika kaunti hizo tatu, zirejelee masomo ya kawaida kuanzia Julai 20, 2023,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Waziri Kithure Kindiki (Usalama) na Ezekiel Machogu (Elimu).

Taarifa hiyo ilisema kuwa serikali imechukua hatua za kutosha kuhakikisha usalama wa wananchi na wanafunzi katika shule zote humu nchini.

Mnamo Jumanne, wizara hizo mbili zilikuwa zimeagiza kwamba wanafunzi wote wa shule za kutwa katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Kisumu wasalie nyumbani kwa hofu kwamba wangeathiriwa na maandamano dhidi ya serikali yaliyoitishwa na Azimio siku tatu; Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.

Wizara hizo zimeamuru wanafunzi warejee shuleni wakati ambapo muungano wa Azimio umetangaza kuwa maandamano yataendelea kote nchini Alhamisi, Julai 20, 2023.

Kwenye taarifa kinara mwenza wa muungano huo Martha Karua aliwapongeza wafuasi wao waliojitokeza kwa wingi kushiriki maandamano ya Jumatano, Julai 19, 2020.

Aidha, alilaani maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano: Jinsi polisi walivyozima mkakati wa Mwangi Wa...

Kumbe nyinyi ni ‘wangwana’, Kindiki awaambia...

T L