• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Maandamano: Jinsi polisi walivyozima mkakati wa Mwangi Wa Iria

Maandamano: Jinsi polisi walivyozima mkakati wa Mwangi Wa Iria

NA MWANGI MUIRURI 

MAAFISA wa polisi waliweka vizuizi vya barabara katika miji ya Murang’a na Kabuta ili kumzuia aliyekuwa Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria kuingia kuongoza maandamano.

Duru za ujasusi zilikuwa zimefichua kwamba Bw Wa Iria alikuwa ameonekana katika kaunti ndogo ya Gatanga akijiandaa kuelekea jiji kuu la kaunti na ndipo vizuizi vikawekwa.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi alisema kwamba “tulipata habari kwamba washukiwa hao wa kufathili maandamano huenda wakapitia mji wa Kenol mwendo wa saa Tano asubuhi na ndipo tulijiweka chonjo kuwakabili”.

Aidha, aliyekuwa diwani maalum Bw Habire Chege alienda mafichoni baada ya kupata fununu kwamba maafisa wa usalama walikuwa wakimwinda.

Bw Chege aliyekuwa ameonekana katika eneo la Huhi lililoko katika viunga vya mji wa Murang’a alihepa ghafla baada ya kupata fununu kwamba maafisa wa usalama walikuwa wanamlenga.

“Mimi niko tu katika sehemu fulani hapa Murang’a lakini kwa sasa siwezi nikachomoka kutoka mafichoni kwa sababu nina fununu kuhusu mipango ya maafisa hao kutaka kunitia mbaroni,” akasema.

Bw Wa Iria na Bw Chege ndio wamekuwa wakishirikisha maandamano hayo ya Azimio katika Kaunti ya Murang’a, wiki jana wakizindua hafla ya ukusanyaji saini za kumtimua Rais William Ruto mamlakani.

Hata hivyo, hakuna kipengele chochote cha kisheria ambacho husema saini za raia zinaweza kumng’atua Rais mamlakani.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Patrick Mukuria alisema kwamba “Murang’a kumetulia, tuko macho na visa vya kuharibu amani havitavumiliwa kamwe”.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba “hapa kwetu hatutakubali pageuzwe ngome ya kuhujumu uchumi na serikali”.

Alisema kwamba eneo la Kati limebarikiwa kwa sasa kwa kuwa “tumevuna mahindi, mchele, maharagwe na viazi na bei ya chakula kwa sasa haitusumbui”.

  • Tags

You can share this post!

Walinzi warejeshwa kwa makazi ya Mama Ngina Kenyatta

Serikali yaagiza masomo kurejelewa Nairobi, Mombasa na...

T L