• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Serikali yaondoa hitaji la vitambulisho kwa wanafunzi kuomba mikopo ya elimu ya juu

Serikali yaondoa hitaji la vitambulisho kwa wanafunzi kuomba mikopo ya elimu ya juu

NA CHARLES WASONGA 

SASA wanafunzi ambao hawajatimiza umri wa miaka 18 wanaweza kutuma maombi na kupokea mikopo na ufadhili wa aina nyingine yoyote kupiga jeki elimu yao ya vyuo vikuu.

Hii ni baada ya Baraza la Mawaziri Jumanne kuondoka hitaji kwamba sharti wanafunzi wawe na vitambulisho vya kitaifa kabla ya maombi yao ya ufadhili kushughulikiwa.

Juzi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwamba wanafunzi ambao hawana vitambulisho vya kitaifa wanaweza kutuma maombi ya ufadhili lakini hawatapewa hadi pale watakapowasilishwa vitambulisho vya kitaifa.

“Kuna ujumla, wanafunzi 1,900 ambao wameitwa kujiunga na vyuo vikuu lakini hawajatimiza umri wa miaka 18. Kwa hivyo, hawana vitambulisho vya kitaifa. Wanafunzi kama hawa wataruhusiwa kuwasilisha maombi lakini mikopo yao haitatolewa hadi pale watakapowasilisha nambari zao za vitambulisho vya kitaifa,” Bw Machogu akawaambia wabunge wanachama wa kamati Alhamisi wiki jana katika majengo ya bunge.

Waziri alisema hayo akijibu malalamishi kutoka kwa wabunge Martha Wangari (Gilgil) na Jared Okello (Nyando) kwamba sio haki kwa Serikali kuwanyima wanafunzi wasiotimu umri wa miaka 18 mikopo kwa misingi ya umri wao.

Lakini sasa wanafunzi hao wamepata afueni baada ya Baraza la Mawaziri kuondoa hitaji kwamba sharti wanafunzi wawe na vitambulisho vya kitaifa kabla ya kuomba mikopo kutoka kwa Bodi ya Kufadhili Masomo katika Vyuo Vikuu (HELB).

“Wizara ya Elimu na wadau wengine wanaagizwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi sawa na kuomba na kupata mikopo na aina nyingine za ufadhili haraka iwezekanavyo,” ikasema taarifa kutoka kwa Ikulu ya Rais baada ya mkutano huo wa Baraza la Mawaziri.

Mkutano huo uliongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu Ndogo ya Kakamega wakati huu ambapo kiongozi wa taifa yuko katika ziara ya siku tano katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Mwanadada ahadithia alivyojipata jela kwa mauaji ya mumewe...

Utata Gabon wanajeshi wakifuta matokeo ya urais

T L