• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Serikali za kaunti zadai mabilioni, shughuli za kaunti hatarini

Serikali za kaunti zadai mabilioni, shughuli za kaunti hatarini

NA MARY WANGARI

MTINDO wa kuchelewesha mgao wa fedha umetajwa kama kiini cha ufisadi na kuhatarisha ugatuzi huku kaunti zikiwa bado hazijapokea kiasi cha zaidi ya Sh94 bilioni miezi miwili tu kabla ya bajeti ya mwaka huu kukamilika.

Serikali za kaunti zote 47 nchini zingali zinasubiri jumla ya Sh94.35 kutoka kwa Hazina Kuu hali inayotishia kulemaza shughuli za kaunti ikiwemo miradi ya maendeleo na malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wa kaunti.

Fedha hizi zinajumuisha malimbikizi ya miezi mitatu ambayo ni pamoja na Sh31.45 bilioni za Februari, Sh29.6 bilioni na Sh33.3 bilioni kwa miezi ya Machi na Aprili mtawalia, Seneti ilielezwa Jumatatu katika kikao cha Kamati inayosimamia Fedha za Umma na Hazina Maalum.

Akizungumza mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi kama mwenyekiti, Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u alisema kuwa Hazina Kuu inadaiwa jumla ya Sh306 bilioni.

Kiasi hiki cha pesa kinajumuisha mgao wa Sh94.35 ambazo hazijalipwa kwa serikali za kaunti pamoja na Sh211.6 bilioni zinazodaiwa na serikali kuu, alifafanua Waziri.

Kufikia sasa serikali za kaunti zingali zinasubiri mgao wa Sh31.45 bilioni kwa  Februari, Sh29.6 bilioni na Sh33.3 za Machi na Aprili mtawalia, kulingana na taarifa iliyowasilishwa kwa Seneti.

Huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya bajeti kukamilika, serikali za kaunti bado hazijapokea asilimia 25 ya mgao wa fedha ikilinganishwa na asilimia 10 pekee inayodaiwa na serikali kuu.

Akijibu maswali kuhusu ucheleweshaji wa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti, Waziri Ndung’u alikuwa na wakati mgumu kufafanua sababu ya kuwepo tofauti hiyo.

Seneti imeelezea wasiwasi wake kuhusu ucheleweshaji huu wa kila mara huku ikitilia shaka kujitolea kwa serikali kufanikisha ugatuzi.

Wakiongozwa na Seneta wa Migori, Eddy Oketh, maseneta wameishutumu serikali kwa kukiuka Katiba na kuhatarisha ugatuzi.

Katiba katika Kifungu 219 inasema kuwa, “mgao wa kaunti kutokana na mapato yanayokusanywa na serikali kuu utasambaziwa kaunti pasipo kucheleweshwa au kupunguzwa, isipokuwa tu wakati usambazaji huo umesitishwa kuambatana na Kifungu 225.”

“Ucheleweshaji wa mgao wa fedha ni kero kubwa. Sasa tumebakisha miezi miwili pekee katika bajeti ya mwaka huu na kaunti bado hazijapokea asilimia 58 ya fedha zinazostahili kupokea,” alisema Seneta Osotsi.

“Kando na kulemaza miradi ya maendeleo katika kaunti na malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wake, ucheleweshaji wa mgao wa fedha ndio chanzo cha ufisadi unaotekelezwa kabla ya kufunga bajeti.”

Aidha, waundasheria hao walihoji sababu ya Hazina Kuu kutopatia serikali za kaunti kipaumbele ikizingatiwa kwamba kiwango cha mgao wa kaunti ni cha chini ikilinganishwa na cha serikali kuu.

Huku akitaja nyakati ngumu kiuchumi zinazokabili taifa, Waziri alisema kuwa kaunti zitapokea malimbikizi ya mgao wa fedha kwa awamu kuanzia na malipo ya Februari yatakayotolewa katika muda wiki moja kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Hatukiuki sheria kimaksudi. Ucheleweshaji huu unatokana na changamoto kali zinazotukabili. Tunapaswa kutuma pesa kwa kaunti kufikia tarehe 15 lakini nyakati ni ngumu hali ambayo imevurugwa zaidi na upungufu kwenye mapato yanayokusanywa na deni kubwa linalotuandama,” alisema Waziri.

Kuhusu suala la ushuru kama moja kati ya mikakati ya Hazina Kuu ya kuongeza mapato, waundasheria wakiongozwa na Seneta wa Narok walionya kwamba hatua hiyo huenda ikahujumu uwekezaji nchini na kuwalazimu wawekezaji wa kigeni kufunganya virago.

Hata hivyo, huku Hazina Kuu ikilalamikia upungufu wa mapato yanayokusanywa nchini, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ilikiri kupiku malengo yake ya ukusanyaji ushuru kwa mara nyingine katika bajeti ya 2021/2022 kwa zaidi ya Sh114 bilioni.

“Ni kweli tulipita malengo yetu kwa asilimia 8.2. Tulikusanya Sh114 bilioni zaidi kufikia mwisho wa bajeti iliyokamilika Juni 30, 2022 ikilinganishwa na kiasi tulichokusanya mwaka jana,” Kamishna wa Masuala ya Sheria KRA, Paul Mutuku alieleza Kamati.

  • Tags

You can share this post!

Adhabu ya kunyongwa yashtua washtakiwa  

Akothee na Andrew Kibe wakabana koo

T L