• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Akothee na Andrew Kibe wakabana koo

Akothee na Andrew Kibe wakabana koo

Na MERCY KOSKEI

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amemkashifu vikali Andrew Kibe kwa kuchambua watu mashuhuri kila mara, akimwonya kuwa huenda akachukuliwa hatua za kisheria.

Akothee alisikitika kwamba kile ambacho Kibe anafanya sio sanaa bali ni kukosa heshima hasa kwa wanawake.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Akothee alimshutumu mtangazaji huyo wa zamani wa redio kwa kupotosha kizazi cha sasa kwa kile alichokitaja kama “kampeni inayolenga kupaka wengine matope kupitia video zake”.

Mama huyo wa watoto watano hakukomea hapo, aliendelea kusema kuwa Kibe ni mtu mwenye uchungu na wivu wa maendeleo hasa ya watu wengine kwani watu wanastawi katika maeneo aliyoshindwa.

Akothee alisema kuwa mtangazaji huyo wa zamani wa NRG Radio na Kiss FM ni mtu aliyefeli na hufurahia kuwatusi wengine.

“Andrew Kibe kuwa mwangalifu usiruhusu unachokifanya kukusukuma jela. Hauko juu ya sheria na kuamka tu na kupiga kelele. Sote tunaelewa kuwa una wivu kwa yeyote anayefanya vizuri kwa  maisha , unaweza kuunda aina zote za video zako lakini sitakuruhusu uendelee kuumiza watu,” alisema.

Mwanamuziki huyo aliashiria kukerwa na dai la Kibe, aliyefananisha masuala yake ya ndoa na video tata inayohusishwa na Waziri Msaidizi (CAS) Wizara ya Usalama, Millicent Omanga.

Akothee aliendelea kusema kuwa Kibe ni Mkenya aliyekimbilia nchi ya Amerika kujificha baada ya kufeli akimshtumu vikali kuwa wanaume wenzake wanafanya kazi huku yeye akifuatilia maisha ya watu.

Hata hivo, alimtaka Kibe kuchapisha mitandaoni hali ya anavyoishi kwa muda wa wiki moja ikiwa kweli anaendelea vizuri Amerika na pia bili anazolipa.

“Wewe ni mtu uliyeshindwa maishani, kwa hivyo unaona maisha yako ndani ya mafanikio ya watu wengine.Yeyote anayemfuata Kibe lazima awe  na tabia kama zake. Tutakurudisha Kenya ujibu maswali yote unayouliza. Ni lazima uwajibike kwa matendo yako,” aliandika

Alimwyonya dhidi ya kushambulia familia za wengine kwa kuamrisha DNA kufanywa ili kubaini wazazi kamili akisema kuwa watoto ndio huumia hapo baadaye.

Mashambuliano ya wawili hao yanajiri siku chache baada ya Akothee kufunga pingu za maisha na mumewe mzungu, Dennis Schweizer aliyembandika jina la utani kama ‘Omosh’.

  • Tags

You can share this post!

Serikali za kaunti zadai mabilioni, shughuli za kaunti...

MAPISHI KIKWETU: Saladi ya karoti na mananasi

T L