• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Sheria mpya: Wanaouza pombe haramu kuona cha mtema kuni

Sheria mpya: Wanaouza pombe haramu kuona cha mtema kuni

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kirinyaga Bi Njeri Maina ametoa onyo kali kwa wanaouza pombe haramu nchini, akisema ‘siku zao zinaekelea ukingoni’.

Akielezea kusikitishwa kwake na kero ya pombe haramu ambayo kwa kiasi kikubwa imelemea vijana, mbunge huyo wa chama cha UDA amefichua kwamba kuna mapendekezo kurekebisha sheria kudhibiti utengenezaji na uuzaji wa pombe nchini.

“Hivi majuzi tumefanya mkutano na Naibu Rais Rigathi Gachagua na madiwani kutoka eneo la Mlima Kenya Naivasha, ambapo tuliafikiana tubadilishe sheria za kudhibiti utengenezaji na uuzaji wa pombe kwa manufaa ya nchi yote,” Bi Maina aliambia Taifa Leo, kupitia mahojiano ya kipekee.

Mbunge huyo aidha alifafanua kwamba serikali za kaunti zote zitajadili na kubuni sheria za kudhibiti utengenezaji na uuzaji wa pombe.

Ikitiliwa maanani unywaji wa pombe za bei rahisi umeathiri vijana kote nchini, Bi Maina alisema shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (Kebs) litafungua afisi kila kaunti kupima bidhaa zote zinazouziwa wananchi.

Bi Maina aliambia Taifa Leo hivi “hakuna muuzaji pombe atakubaliwa kufungua kilabu pasipo idhini ya umma.”

Alisema bodi za kuidhinisha utoaji wa leseni za kuuza pombe zitatolewa tu katika eneo ambapo wananchi wanataka.

Wenye viwanda vinavyotengeneza pombe lazima vitimize masharati yaliyowekwa na Kebs.

“Mtengeneza pombe isiyofikia kiwango kitakachowekwa na Kebs atafunga virago na kwenda nyumbani,” Bi Maina alisema.

Mwakilishi huyo wa kaunti alisema vilabu vinavyouza pombe isiyo ya bei ya juu vya Wines & Spirits vitadhibitiwa na wananchi watakaokuwa na usemi mkuu.

“Wananchi ndio watakaosema iwapo wanataka kilabu katika maeneo yao au la.”

Unywaji pombe umesababisha familia nyingi kutengana na maelfu ya watu kufariki.

Pia pombe hizi zimesababisha walevi wengi kuwa vipofu na familia zingine kutengana.

Maeneo ya mashambani yameathirika pakubwa kwa vile wavulana wamekataa kuoa na kuhatarisha kusambaratika kwa familia.

“Hakuna wanaume wa kufunga ndoa na wasichana siku hizi katika baadhi ya maeneo. Nguvu za kiume zimeathiriwa na pombe hizi sisizoidhinishwa na Kebs,” alisema mwanasiasa huyo.

Bi Maina alisema sasa serikali imeweka mikakati ya kuokoa jamii dhidi ya pombe hizi.

Idadi ya wanaopata ajira kutokana na vilabu na makampuni ya kutengeneza mvinyo itazingatiwa pia.

Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua ameapa kuzima kero ya pombe haramu katika ngome yake, Mlima Kenya, akisema oparesheni hiyo pia itaelekezwa maeneo mengine nchini.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa wizi wa baiskeli

Mfalme Charles III kuongoza nchi 15

T L