• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Shughuli ya ufukuaji makaburi Shakahola yatatizwa na mvua kubwa

Shughuli ya ufukuaji makaburi Shakahola yatatizwa na mvua kubwa

NA ALEX KALAMA

SHUGHULI ya ufukuaji makaburi ili kutoa miili ya watu ambao inadaiwa waliangamia kwa kufuata imani potovu katika msitu wa Shakahola Ranch ulioko Chakama katika Kaunti ya Kilifi ilisitishwa kwa muda, baada ya mvua kubwa kunyesha Ijumaa.

Maafisa wanaoendesha operesheni hiyo kwenye shamba linalodaiwa kuwa la mhubiri Paul Mackenzie mnamo Alhamisi walifukua miili 11 ambapo mili mitano ilikuwa ya watoto huku miili sita ikiwa ya watu wazima kutoka kwa makaburi 10 na kufanya idadi ya waliofariki kugonga 109.

Hata hivyo maafisa wakuu wa serikali akiwemo Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki mnamo Ijumaa akiwa Shakahola alisema anasikitishwa sana na hali na yaliyotokea huko.

“Sijui ni ‘mungu’ gani wanayezungumzia. Wameweka mauaji mbele. Hawa watu ni waongo hawaabudu Mungu bali ni magaidi. Na tutawachukulia hatua kali kama vile tunavyochukulia magaidi wengine na majangili wezi wa mifugo kule kaskazini mwa Bonde la Ufa,” alisema Prof Kindiki.

Naibu Inspekta wa polisi wa Utawala Noor Gabow na mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai, mkuu wa ofisi ya uchunguzi Abdalla Komesha ni miongoni mwa wale walioandamana na waziri huyo.

Aidha shughuli ya upasuaji wa maiti hizo za wahanga wa imani potovu itaanza juma lijalo chini ya uangalizi wa maafisa wa polisi na itafanywa na wanapatholojia wa serikali pekee ambapo shughuli hiyo itafanyika katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi.

Kando na hayo ni kwamba idadi ya watu waliookolewa tangu kuanza kwa operesheni hiyo imefika 34.

  • Tags

You can share this post!

Ndege kutumika katika operesheni Shakahola

Raila sasa atangaza maandamano upya

T L