• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Tahadhari mafuriko yakiua 3 Makueni

Tahadhari mafuriko yakiua 3 Makueni

PIUS MAUNDU na COLLINS OMULO

MVUA inayonyesha sehemu kadhaa nchini imesababisha maafa baada ya watu watatu kusombwa na mafuriko katika Kaunti ya Makueni, huku tahadhari ikitolewa kuwa itaongezeka katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Kati ya watatu hao, wawili walisombwa na mafuriko kwenye Mto Thange huku mwendeshaji bodaboda akifariki Mto Kaluku ulipovunja kingo zake.

Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Bw Mohamed Maalim amewaonya wakazi wanaoishi karibu na mito mbalimbali kuwa makini kuepuka hatari.

“Miili ya watu hao watatu haijapatikana. Waliojitolea kuutafuta mwili wa mwendeshaji bodaboda aliyesombwa na maji Jumapili hawajafanikiwa. Hata hivyo, walipata shati lake. Mtu yeyote asijaribu kuvuka hata vijito na mito wakati huu wa mvua,” akasema Bw Maalim.

Idara ya Kutabiri Hali ya Hewa nchini imetahadharisha Wakenya kujitayarisha kwa baridi ikieleza kuwa mvua bado itazidi kwa wiki moja ijayo huku kiwango cha joto kikishuka hadi nyuzi sita katika baadhi ya maeneo nchini.

Hii ni kwa sababu upepo mkali unatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ilieleza.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilisema kiasi cha mvua katika maeneo mengi ya nchi kimekuwa kikiongezeka tangu Novemba 15, 2021.

Kulingana na utabiri wa hivi punde uliotolewa jana, mvua itaendelea kunyesha katika maeneo kadhaa ya nchi huku nyanda za juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, nyanda za chini Kusini Mashariki na Pwani, zikitarajiwa kupata mvua kubwa kati ya milimita 20 na 50.

Hali hii itashuhudiwa katika Kaunti za Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, na Tharaka Nithi, Machakos, Kitui, Makueni, Kajiado na Taita Taveta.Kaunti za Kisii, Nyamira, Trans-Nzoia, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Kericho, na Bomet zitapata mvua alasiri na ngurumo za radi huku usiku kukiwa na mawingu kiasi na asubuhi hali kavu kwa ujumla.

Kaunti za Kakamega, Vihiga, Bungoma, Pokot Magharibi, Siaya, Kisumu, Homa Bay, Busia, Migori, Baringo, Nakuru, Narok na Laikipia pia zitakumbwa na hali hiyo ya hewa.

Kaunti za Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale zitapata mvua asubuhi na alasiri.

Kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zitapata mvua za asubuhi na manyunyu alasiri.

“Kiwango cha mvua kinaweza kupungua kadri muda wa utabiri unavyoendelea. Mvua ya alasiri na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache. Usiku kuna uwezekano wa kuwa na mawingu kiasi,” ripoti ya utabiri wa hali ya hewa ilionyesha.

Kwa kaunti za kaskazini Magharibi mwa Kenya za Turkana na Samburu, mchana kutakuwa za jua na uwezekano wa mvua za mara kwa mara kutokea katika maeneo machache.

You can share this post!

Safari za treni kwa Nyanza, Magharibi sasa zanukia

Koo 7 zasaka maafikiano kabla uchaguzi

T L