• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Tume ya Rais Ruto kuhusu uchunguzi Shakahola yazimwa na Mahakama Kuu

Tume ya Rais Ruto kuhusu uchunguzi Shakahola yazimwa na Mahakama Kuu

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu imepiga breki tume iliyoteuliwa na Rais William Ruto kuchunguza mauaji ya watu zaidi 200 katika shamba la Muhubiri Paul Mackenzie.

Tume hiyo inayoongozwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jessie Lesiit imeagizwa na Jaji Lawrence Mugambi isitishe mara moja zoezi hilo hadi pale kesi iliyowasilishwa na kinara wa chama cha Azimio Raila Odinga itakaposikizwa na kuamuliwa.

Akisitisha utendakazi wa jopo hilo, Jaji Mugambi alisema asasi nyingine za serikali zinazojumuisha polisi, kamati ya bunge la seneti ikiongozwa na Seneta wa Tana River Danson Mungatana na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu (KNCHR) zinachunguza mauaji hayo ya wakristo waliofundishwa itikadi kali na Pasta Mackenzie.

Akasema Jaji Mugambi, “Kamati hizi zote zinatumia pesa za umma na vile vile jopo la Jaji Lesiit litakuwa linatumia pesa za umma. Huu utakuwa ni uharibifu mkubwa wa pesa za umma.”

Pia Jaji Mugambi alisema Rais Ruto aliteua tume hiyo kinyume cha sheria na bila ya kumshauriana na Jaji Mkuu Martha Koome.

Azimio kupitia wakili Paul Mwangi ilihoji hatua ya Rais Ruto kuteua tume za kuchunguza suala lolote lile kuteuliwa pasipo kushirikisha tume ya huduma za mahakama (JSC) iliyopewa mamlaka ya Kikatiba kufanya teuzi hizo kutamvimbisha kichwa pamoja na marais watakaomfuata kuvunja sheria wapendavyo.

Azimio pia ilimkosoa Rais Ruto kwa kukaidi Katiba kwa kujitwika mamlaka asiyo nayo.

Azimio ilieleza mahakama tabia hiyo ya Rais Ruto ya kuteua majaji kuongoza majopo ni kuingilia na kuvuruga uhuru wa utendakazi wa idara ya mahakama na uhuru wa majaji.

Jopo hilo liliteuliwa kuchunguza mauaji ya watu zaidi 200 katika shamba la Muhubiri Paul Mackenzie.

“Uteuzi wa jopo/tume hiyo unakinzana na Katiba kwa vile sasa Rais Ruto na marais watakaomfuata watakuwa na tabia ya kuwashawishi majaji kwa kuwapa kazi kubwa na pesa nono kutweza utendakazi wao na kuwafanya kutoa maamuzi yanayoegemea upande mmoja,” Mwangi alifafanua akiomba tume hiyo ipigwe kalamu.

Azimio iliomba mahakama itangaze kwamba hatua hiyo ya Rais Ruto inakinzana na Katiba na kwamba amejinyakulia mamlaka asiyopewa na mamlaka.

Jaji huyo alisema atakuwa anakosa endapo ataruhusu tume hiyo ya Jaji Lesiit kuanza utendakazi kabla ya kesi inayopinga uamuzi wa rais kusikizwa na kuamuliwa.

Rais Ruto aliteua jopo hilo la wanachama wanane mnamo Mei 4, 2023 kuchunguza mauaji ya halaiki ya wafuasi wa kanisa la Pasta Mackenzie, eneo la Shakahola.

Pia tume hiyo ilikuwa ichunguze baadhi ya makanisa na viongozi wao na kutoa pendekezo kuchuja mapasta ambao hawajahitimu.

 

  • Tags

You can share this post!

‘Nabii Yohana wa Tano’ aitwa afike mbele ya...

JIPENDE: Tabia zinazoonyesha mja hajiamini

T L