• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ufisadi: EACC yataka KPA ichukuliwe hatua

Ufisadi: EACC yataka KPA ichukuliwe hatua

Na VALENTINE OBARA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), bado inasubiri uamuzi wa Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa madai ya ufisadi wa mamilioni ya pesa katika Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) mjini Mombasa.

Kulingana na EACC, mojawapo ya uchunguzi uliofanywa na maafisa wake unahusu madai kuwa KPA ilitumia Sh137.6 milioni kununua maji katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 kwa njia zinazokiuka sheria.Kwenye ripoti ambayo imechapishwa katika gazeti rasmi la serikali, EACC imesema kuwa kampuni zilizodaiwa kupokea fedha hizo ni Samnix Enterprises, Mombasa Fresh Water Supply Company, Pincho Traders, Smech Enterprises, Nyavu Traders na Aquisana Limited.

Ripoti hiyo ilitiwa sahihi na Mwenyekiti wa EACC, Askofu Mkuu Mstaafu Eliud Wabukala, na Afisa Mkuu Mtendaji Twalib Mbarak. Imetolewa siku chache baada ya madai mengine kuibuka kuhusu njama za maafisa wa bandari kusaidia waagizaji mizigo kukwepa ushuru.

EACC ilisema ilianzisha uchunguzi huo punde baada ya kupokea malalamishi kuhusu madai ya ufisadi katika ununuzi wa maji bandari ya Mombasa mnamo Septemba 19, 2018.“Uchunguzi ulibainisha kuwa KPA haikufuata sheria iliposhirikiana kibiashara na makampuni hayo sita na kupelekea hasara ya pesa za umma Sh136.6 milioni.

Uchunguzi zaidi ulibainisha kuwa baadhi ya makampuni yalilipwa kwa bidhaa ambazo hazikupokewa,” ripoti hiyo ikasema.Tume hiyo inasema iliwasilisha ripoti kwa DPP mnamo Septemba 7, mwaka huu, ikipendekeza kuwa mashtaka yafunguliwe dhidi ya maafisa wa KPA na wakurugenzi wa makampuni yaliyodaiwa kuhusika kwa sakata hiyo.

Kando na hayo, EACC imesema pia ingali inasubiri majibu ya DPP kuhusu madai ya ufisadi wa zabuni ya kununua na ukarabati wa mtambo wa kusambaza gesi (compressor) uliogharimu Sh8.4 milioni.Kwa mujibu wa ripoti ya tume hiyo, bei ya mtambo huo haikutakiwa kupita Sh8 milioni.

Madai kuhusu ufisadi katika zabuni hiyo iliyopeanwa kwa kampuni ya M/S Alootek yalianza kuchunguzwa baada ya malalamishi kupokewa na EACC mnamo Januari 21, 2019.“Mnamo Septemba 1, 2021, ripoti iliandikwa ikawasilishwa kwa DPP ikiwa na mapendekezo kwamba maafisa wa KPA, wakurugenzi wa Alootek Systems Ltd na kampuni ya Allotek Systems Ltd washtakiwe,” ikasema ripti ya EACC.

Imesemekana kuwa, uchunguzi ulibainisha KPA haikufuata sheria ilipotoa zabuni hiyo kwani ilikubali ombi la kampuni hiyo kutaka zabuni bila kutoa nafasi kwa ushindani kutoka kwa mashirika mengine ambayo huenda yangetoza bei ya chini.

Zaidi ya hayo, tume hiyo imedai kuwa uchunguzi ulionyesha kuwa kampuni hiyo ilidanganya KPA kwamba hakuna kampuni nyingine inayouza aina ya mtambo ambao shirika hilo la serikali ilikuwa inataka kununua.Miongoni mwa mashtaka ambayo yamependekezwa ni ukiukaji wa sheria husika za ununuzi wa bidhaa za mashirika ya serikali, utumizi mbaya wa mamlaka, miongoni mwa nyingine.

EACC huchapisha ripoti kila robo ya mwaka kuhusu kesi ambazo imewasilisha kwa DPP, na hatua zilizopigwa kufikia sasa.Ripoti iliyochapishwa inahusu kipindi cha kuanzia Julai 1 hadi Septemba 30, mwaka huu.Kulingana na sheria, tume hiyo hutakikana kuziwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu ambaye atahitajika kuziwasilisha kwa Bunge la Taifa.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto, Moi wasihadae wahanga wa Mau...

Wapiganaji wapora chakula cha msaada

T L