• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:54 PM
Uhaba wa meli wachelewesha Wakenya kubobea kwa maswala ya baharini

Uhaba wa meli wachelewesha Wakenya kubobea kwa maswala ya baharini

NA MAUREEN ONGALA

MAMLAKA ya Bandari nchini (KPA) imeeleza kuwa Wakenya hawajajiendeleza kitaaluma jinsi inavyotakikana, kutokana na uhaba wa meli hapa nchini.

Afisa wa mawasiliano wa KPA Bw Hajji Misemo, alisema kuwa licha ya hatua zilizopigwa kuimarisha mapato ya uchumi wa baharini, bado kuna changamoto hiyo ya uhaba wa meli, ambayo alisema inastahili kuchukuliwa kwa uzito.

Akizungumza na Taifa Jumapili wakati wa warsha ya mafunzo kwa wanahabari kuhusu maswala ya uchumi wa baharini iliyoandaliwa na Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) katika hoteli moja mjini Mtwapa, Bw Misemo alikiri kuwa iwapo kampuni ya meli nchini – Kenya Shipping Line – itawezeshwa kununua meli, itasaidia Wakenya kunuifaika kikamilifu kimasomo.

“Meli zimekuwa adimu lakini ukweli unasalia kwamba mwanafunzi lazima aende baharini kwa muda fulani,” akasema.

Wakati huo huo, afisa huyo alisema wanafunzi wanaosomea maswala ya unahodha na wahandisi wa meli hukabiliwa na changamoto ya kufanya mazoezi ya kazi zao.

Kulingana na Bw Misemo, licha ya Kenya kuanzisha mafunzo kwenye vyuo kuwewawezesha Wakenya kupata ajira zinazohusu maswala ya baharini, bado wanafunzi hawajaweza kujiendeleza kimasomo kikamilifu.

“Bandari Maritime Academy ina uwezo ya kuwapa mafunzo maelfu ya manahodha na mabaharia, lakini kabla ya kutuzwa vyeti vya unahodha ni lazima wawe wameeenda baharini kwa muda fulani kujua jinsi ya kuendesha chombo,” akasema.

Alisema KPA inashirikiana na kampuni kadha nchini kutatua changamoto hiyo lakini juhudi hizo bado hazijafua dafu.

“Ipo haja kwa serikali kuanza kufikiria mikakati ya kutafuta meli zetu wenyewe kama Wakenya,” akasema.

Bw Misemo alitoa wito kwa wadau kujitolea kusaidia Wakenya kuafikia malengo yao ya kufaidika na kuimarisha maisha yao kupitia uchumi wa baharini.

“Japo serikali ina mikakati, inatakikana tupige hatua sisi wenyewe na tuanze kupata meli zetu. Mabaharia wawe ni wetu na iwe itapatikana fursa ya mafunzo ya hali ya juu, kuajiri vijana wetu na kupanua uchumi wetu,” akasema.

Alitoa mfano na kusema kuwa miaka ya nyuma mataifa ya Afrika Mashariki yalikuwa na meli ambazo zilitumika katika Ziwa Victoria na hata kuenda ng’ambo. Wakati huo mabaharia wengi walijunzia kazi hapo.

Kwenye warsha hiyo, Bw Misemo aliwapa changamoto vijana katika jamii kujitokeza kupata masomo kuhusu taaluma hiyo muhimu.

“Bandari haiwezi kuajiri kila mtu lakini ipo haja ya watu kuanza kukumbatia uchumi wa baharini na kujifunza kwa mfano kujenga meli kwa sababu ni sekta ambayo inapanuka sana,” akasema.

Mshirikishi wa MCK eneo la Pwani Bi Maureen Mudi, alisema kuwa wanaendeleza mikakati ya kuanzisha mafunzo maalum kwa wanahabari waelewe namna ya kuandaa habari na makala kuhusu maswala ya uchumi wa baharini.

“Tutatafuta watu ambao wamefaulu katika nyanja za uchumi wa baharini kutusaidia kuandika mtaala huo ambao tutatumia kuwafunza katika vyuo ili wawe na ufahamu wa kutosha kuripoti maswala hayo nyanjani,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Ruto: Raila atatulizwa na ofisi ya upinzani

KINAYA: Gachagua atawaweza nyuki wa Ukambani aliochokoza?

T L