• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
KINAYA: Gachagua atawaweza nyuki wa Ukambani aliochokoza?

KINAYA: Gachagua atawaweza nyuki wa Ukambani aliochokoza?

NA DOUGLAS MUTUA

RIGGY G amechokoza nyuki wa Ukambani!

Anawezaje kuwaambia wamteme mwana wao mpendwa, Kalonzo Musyoka, kama kikohozi?

Watamtema wabaki na nani ilhali amewahakikishia kwamba atamfukuzia Zakayo kijijini Sugoi ifikapo 2027? Watu wana mchezo sana.

Najiuliza: Kwani Riggy G hajui jamii hiyo imepandwa na hasira tangu ichezwe shere na Baba Jimmy alipostaafu na kumwacha Kalonzo na Wakambodia kwenye mataa?

Kwani Naibu Rais, anayedendwa ‘Mkweli’ Mlima Kenya, hajasikia hekaya za jinsi mashemeji zake hao, zamani za kale wakituma nyuki kuwashughulikia wasiokuwa marafiki zao?

Bahati ya Riggy G tu ni kwamba siku hizi wakazi wa eneo hilo kame la mashariki ya nchi hawatumii nyuki kuwakabili maadui zao, wamepiga hatua fulani. Nimesema hatua fulani kwa kuwa sina hakika hatua zenyewe ni za kwenda mbele au kurudi nyuma.

Au kati ya nyuki na mawe, maendeleo ndiyo yepi? Nikidhani mawe yanachosha. Labda sijui. Naambiwa enzi hii ya teknolojia wameachana na ‘teknolojia’ yao ya kale ya kutumia nyuki, wanatumia maandamano, kufoka kwa fujo mitaani, hata mawe wanajua kufurumisha.

Ajabu! Wamehusiana kwa karibu na washirika wao wa kisiasa, wakajua shughuli zinavyofanywa katika Upinzani, sasa wanaandaa maandamano hata Kitui ndani! Bado hawajajua kung’oa reli, na naomba wasiwahi kujua kabisa kwa kuwa ile ya mwendo wa kadiri iitwayo SGR inapitia maeneo yao, wakifanya hivyo hatufiki Mombasa.

Tutayakosa maji ya chumvi kimchezo tu, wafanyabiashara nao waingie hasara kuu, uchumi uwe hali mahututi, hasira za Zakayo zipandishe nyuzi joto kiasi cha kuchemsha maji ya ugali!

Riggy G naye ataanza kulia eti wafanyabiashara wa mlimani wanaoendesha shughuli zao kati ya Mombasa, Nairobi, Naivasha na Nakuru hawapati biashara. Huo ndio ubora wa nchi yetu, yaani tunategemeana katika kila kitu. Hakuna mtu au eneo linaloweza kujitenga na kujitosheleza mahitaji yake yote, hivyo tuna lazima ya kutunzana.

Tunaweza kuitumia saratani yetu ya ukabila kufaana, si kufanyiana hiana, yaani tutegemeane kujengana, si kubomoana Huko kutegemeana nilikushuhudia mubashara mtaani Mathare, Nairobi, wakati wa machafuko ya mwaka 2007/8.

Makundi mawili hasimu – la waandamanaji na la wenye maduka – yalifanya shughuli zao kwa mpango. Mwenye duka au kibanda alipewa saa chache za kufungua kazi yake, waliofanya fujo wanunue vyakula na vinyaji, kisha machafuko yaanze rasmi. Kila mmoja alitarajiwa kufuata ratiba hiyo, lau sivyo akipatikana pasipo aambiwe ‘hatukujui!’ na kuonyeshwa cha mtema kuni! Riggy G anapaswa kujua kuwa jamii ya Wakambodia, sawa na mjamzito, ina hasira za karibu na haifurahii mzaha kama vile pendekezo la kumtema Kalonzo.

  • Tags

You can share this post!

Uhaba wa meli wachelewesha Wakenya kubobea kwa maswala ya...

Kisanga mimba ya mke wa wenyewe kujiavya akigawa tunda la...

T L