• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Uhifadhi wa Mto Thika walenga kuhakikisha viwango vya maji vinarejea

Uhifadhi wa Mto Thika walenga kuhakikisha viwango vya maji vinarejea

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKLI kwa ushirikiano na washikadau na mashirika yasiyokuwa ya serikali, imejitolea kubuni mikakati ya kurejesha maji katika Mto Thika.

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika katika uboreshaji wa mimea ya wakulima kutoka kaunti za Kiambu, Murang’a na Machakos na viwanda kadha vilivyoko katika mji wa Thika na vitongoji vyake.

Mamlaka ya Kudhibiti Usamazaji Maji ya Water Regulatory Authority (WRA), imezindua mikakati ya jinsi ya kurejesha maji mengi katika mto Thika.

Mradi huo pia umefadhiliwa na nchi ya Uholanzi upitia shirika la Embassy of Earth ambalo lina ujuzi wa kurejesha mito iliyokauka kwa upanzi wa miti kando ya maeneo hayo.

Uchafu unaotupwa kiholela kutoka kwa viwanda kadha maeneo tofauti ndicho chanzo kikuu cha kusababisha uchafuzi katika mto huo.

Mkurugenzi wa WRA, Bw Mohamed Shurie aliyehudhuria hafla iliyofanyika katika kampuni ya Delmonte, Thika, alisema serikali na washika dau wengine imejitolea kuona ya kwamba mto Thika unarejesha ubora wake na kuwa na maji safi.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba mpango huo unazindiliwa haraka iwezekanavyo ili kuhifadhi mazingira,” alisema Bw Shurie.

Alisema mpango huo utahusisha washika dau wote pamoja na wamiliki wa viwanda vyote vilivyoko karibu na maeneo ya mto huo.

Pendekezo hilo liliungwa mkono na  mkurugenzi mkuu wa Athi Water Works Development Agency, Bw Michael Thuita, aliyesema kuwa washikadau wote  kaunti ya Kiambu, na Halmashauri ya Mazingira (NEMA) watashirikiana pamoja kuona ya kwamba mpango huo unafanikiwa bila kushindwa.

“Tutahakikisha mazingira yanarejeshwa kwa hali yake ya hapo awali ili hata mito yetu iweze kurejelea ubora unaostahili,” alisema Bw Thuita.

Mkurugenzi wa shirika la Embassy of Earth, Bw Frank Heckman alisema watakaloangazia zaidi ni kwa nini mto Thika umekabiliwa na chañgamoto tele.

“Tunaelewa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa ambayo imesababisha mto huo kuathirika kimazingira,” alisema Bw Heckman.

Alisema upanzi wa miti utaendelea kwa kishindo kando ya mto huo hasa maeneo ya Gatare, na msitu wa Kimakis katika Kaunti ya Murang’a.

Bi Grace Kuria ambaye ni mwenyekiti wa shirika la Water Resource Users Association (WRUA), alisema shirika hilo litafanya mikutano na wakulima vijijini na wananchi ili kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira hasa mto Thika ambao umeathirika pakubwa.

Sehemu mojawapo ya Mto Thika. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema kilimo kando ya mto huo pia kimesababisha madhara hayo.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Delmonte Bw Stergios Gkalimoutsas alipongeza wageni wote waliokongamana katika kiwanda hicho wakiwa na mipango ya kurejesha hadhi ya mto Thika.

Alisema kampuni hiyo itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na washika dau wengine kufañikisha mpango huo.

Alisema mpango huo pia utazinduliwa maeneo mengine kama Mto Nairobi  baada ya kukamilisha huo wa Thika.
  • Tags

You can share this post!

Muungano wa wachungaji Kilifi wataka wenye mahubiri potovu...

Raila arudi na joto la maandamano

T L