• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Umaskini waongezeka zaidi tangu UhuRuto wachukue madaraka, ripoti zaeleza

Umaskini waongezeka zaidi tangu UhuRuto wachukue madaraka, ripoti zaeleza

NA PETER MBURU

UTAWALA wa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto umezidisha mahangaiko ya Wakenya tangu walipochukua serikali mnamo 2013.

Ripoti za taasisi kuhusu sera na uchumi zinaonyesha kuwa kupitia kwa uongozi wa wawili hao chini ya chama cha Jubilee, idadi ya watu maskini hapa Kenya imeongezeka kutoka asilimia 38.9 Mzee Mwai Kibaki alipowakabidhi madaraka hadi asilimia 53.

Hii ina maana kuwa badala ya kupigana na umaskini jinsi walivyokuwa wameahidi kwenye kampeni zao 2013, wawili hao waliweka sera na mipango ambayo imefanya Wakenya zaidi kuwa maskini zaidi.

Mashirika ambayo yametoa ripoti hizo ni pamoja na Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu (KNBS) ambayo ilisema umaskini nchini uliongezeka zaidi kati ya 2014 na 2018.

Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na athari za janga la Covid-19.

Mashirika mengine ambayo yametoa ripoti kuhusu hali ya kiuchumi miongoni mwa Wakenya ilivyo chini ya UhuRuto ni Kenya Vision 2030, UN Women na Women Count.

Kulingana na Benki ya Dunia, mtu huchukuliwa kuwa maskini iwapo anapata chini ya Sh94 kwa siku.

Kulingana na ripoti hizo, hali ngumu ya kimaisha kwa Wakenya imechangiwa na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya, mzigo wa deni la kitaifa, ongezeko la ushuru na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa idadi ya Wakenya ambao walikuwa wakipokea pesa za kuwakinga na viwango vya juu vya umaskini nayo imeshuka huku walalahoi wakiongezeka.

Kuhusu hali ya chakula, ripoti hizo zinaeleza kuwa uhaba wa chakula bado ni tatizo kubwa kwa Wakenya, ambapo mnamo 2016 kulikuwa na asilimia 19 ya watu ambao walikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula nchini, na asilimia 56 walihangaika kupata mlo.

Juhudi za kuimarisha usalama wa chakula ziliimarika chini ya utawala wa Mzee Kibaki kati ya 2003 na 2012. Lakini tangu alipoondoka madarakani, idadi ya walio na uhaba mkubwa wa chakula imeshuka tu kwa asilimia mbili chini ya Jubilee.

Pia, ripoti hizo zinasema robo ya watoto walio chini ya miaka mitano hawakui ifaavyo kutokana na uhaba wa chakula.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA FA: Man-United yalaza Aston Villa na kufuzu...

TAHARIRI: Chuki: Vigogo wawadhibiti wafuasi wao

T L