• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
TAHARIRI: Chuki: Vigogo wawadhibiti wafuasi wao

TAHARIRI: Chuki: Vigogo wawadhibiti wafuasi wao

Na MHARIRI

SIKU moja tu baada ya Seneta wa Meru Mithika Linturi kukamatwa na maafisa wa polisi kuhusiana na matamshi yake ya kuchochea chuki, kulitokea fujo katika Kaunti ya Bomet jana Jumatatu ambapo viongozi walikuwa wakiandaa mkutano wa Naibu Rais William Ruto.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na gavana wa kaunti hiyo, wabunge na wawaniaji wa viti mbalimbali katika uchaguzi ujao, kilisitishwa ghafla baada ya vijana kuzua vurugu kwa kukiwazuia wanasiasa fulani kuzungumza.

Mtafaruku ulianza wakati Mbunge Mteule wa chama cha ODM Wilson Sossion alipewa nafasi ya kuzungumza na seneta wa Bomet Christopher Lang’at ambapo vijana waliamka kumzuia kuhutu wakidai kwamba yeye (Sossion) hakuwa mmoja wao bali alikuwa mgeno eneo hilo.

Bw Sossion anadaiwa kulenga wadhifa wa seneta wa kaunti hiyo na anatarajiwa kumenyana na wakili Hillary Sigei aliwepo seneta wa sasa Bw Lang’at.

Juhudi za gavana wa Bomet Hillary Barchok kutuliza rabsha za vijana hao hazikufua dafu kwani zilipelekea yeye kukimbilia usalama wake barobaro hao walipomgeukia.

Kisa hiki ni dhihirisho tosha kwamba vijana hao walikuwa wamechochewa na baadhi ya wagombeaji katika eneo hilo. Si ajabu kwamba maenezi ya uchochezi hutokana na wanasiasa wenyewe dhidi ya wanasiasa wanzao wanaoshindania viti husika. Matendo na matamshi ya vijana na wafuasi wa wanasiasa kwa ujum huendana na misimamo na matakwa ya vinara wa vyama vyao.

Ni kutokana na sababu hii ambapo Naibu Rais William Ruto ambaye pia ni kigogo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alijitokeza kuomba msamaha kwa niaba ya seneta Linturi kufuatia matamshi yake alipohudhuria mkutano wa UDA mjini Eldoret Jumamosi.

Naibu Rais bila shaka alilenga kuzuia matamshi ya chuki kusambaa kwenye kampeni siku zijazo, suala ambalo lina uwezo wa kutumbukiza nchi hii katika vita na umwagikaji damu kama ilivyoshuhudia miaka ya 2007/2008.

Bw Ruto pia alizitaka taasisi za kukabiliana na uhalifu na hasa uchochezi ziwakabili washukiwa kwa mujibu wa sheria bila kukubali kutumiwa vibaya kisiasa.

La maana zaidi Naibu Rais aliwataka vigogo wenzake wawadhibiti wafuasi wao wasitoe matamshi yanayohatarisha umoja, amani na utangamano wa taifa hili. Bila shaka, jukumu la kuwaonya na kuwaelekeza wanasiasa linasalia kwa vigogo wa vyama.

Ushauri wa Bw Ruto unafaa kuigwa na vinara wenzake Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Martha Karua kwa kutaja baadhi yao. Viongozi hawa waelewe kwamba bila amani uchaguzi wanaongojea kwa hamu na ghamu hauwezi kuendelea na hakuna mmoja wao angependa kuongoza nchi iliyojaa misukasuko, taharuki na vita.

You can share this post!

Umaskini waongezeka zaidi tangu UhuRuto wachukue madaraka,...

JUMA NAMLOLA: Ababu angefanyia haya rais mwengine, angekuwa...

T L