• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ushoga: Kanisa Katoliki njia panda agizo la Papa likipingwa Afrika

Ushoga: Kanisa Katoliki njia panda agizo la Papa likipingwa Afrika

NA WANDERI KAMAU

MUSTAKABALI wa Kanisa Katoliki uko kwenye njia panda barani Afrika, kufuatia agizo la Papa Francis kwa mapadre katika kanisa hilo kubariki wapenzi wa jinsia moja.

Ingawa lengo kuu la agizo hilo linaonekana kama njia ya kuwavutia washiriki zaidi na kutowabagua watu hao, wachambuzi na wasomi wa masuala ya dini wanasema huenda agizo hilo lilitolewa bila Papa kupewa ushauri wa kina na uongozi wa kanisa hilo.

Kanisa Katoliki lina mamilioni ya washiriki hapa Kenya na barani Afrika kwa jumla.

Kulingana na takwimu kutoka kwa serikali, kanisa hilo ndilo linaloongoza kwa kuwa na washiriki wengi nchini, huku likifuatwa na makanisa ya Kiprotestanti.

Tangu Papa Francis alipotoa agizo hilo, viongozi tofauti wa kanisa wameeleza na kutoa hisia tofauti,  baadhi wakijitokeza wazi kulipinga.

Baadhi ya viongozi wakuu ambao wamejitokeza kulipinga ni kiongozi wa kanisa hilo nchini, Askofu Philip Anyolo, ambaye pia ndiye Askofu Mkuu katika Dayosisi ya Nairobi.

Kulingana na askofu huyo, agizo hilo linakinzana vikali na tamaduni za Kiafrika, hivyo hawataliruhusu.

“Kiafrika, ndoa za jinsia moja hazikubaliki hata kidogo. Ndoa hizo pia zinaenda kinyume na mafunzo ya Biblia,” akasema Askofu Anyolo.

Maaskofu wengine ambao wamejitokeza wazi kupinga agizo hilo ni Cornelius Odiwa wa Homa Bay na mwenzake wa dayosisi ya Eldoret, Askofu Dominic Kimengich.

Askofu Odiwa alisema watafuata msimamo wa Askofu Anyolo, kwani ndiye kiongozi wa kanisa hilo nchini.

Pia, alisema ndoa hizo hazikubaliki kabisa Kiafrika.

Kando na viongozi wa Kanisa Katoliki, watu kutoka dini nyingine pia wameunga mkono pingamizi hizo.

Baadhi yao ni Bw Samuel Kamitha, ambaye ni mwanahistoria na msomi wa masuala ya dini.

Bw Kamitha pia ni mmoja wa waandalizi wakuu wa maombi maalum ambayo hufanyika Desemba 27 kila mwaka karibu na Mlima Kenya.

Mnamo Jumatano, wakati wa maombi hayo, Bw Kamitha alisema hawatakubali hata kidogo tamaduni za kigeni kutumika kuharibu desturi asilia za Kiafrika.

“Tunasimama kidete kupinga uhalalishaji wa ndoa za jinsia moja nchini. Hilo ni jambo linalokinzana kabisa na tamaduni zetu,” akasema.

Maombi hayo yalihudhuriwa na Wakristo, Waislamu, watu wanaofuata dini za kitamaduni kati ya madhehebu mengine.

Kutokana na hisia hizo, wasomi wa masuala ya dini wanasema kuwa mwelekeo huo mpya unafaa kuufungua macho uongozi wa Kanisa Katoliki kuhusu mustakabali wake barani Afrika.

“Kikawaida, maagizo yote kutoka Vatican (makao makuu ya Kanisa Katoliki) huwa hayapingwi hata kidogo. Ni vigumu kusikia usemi au agizo la Papa likikosolewa au kupingwa. Hata hivyo, viongozi kadhaa wanapojitokeza wazi kupinga agizo lake, basi hiyo ni ishara wazi kuwa kuna tatizo kubwa ambalo lazima litatuliwe,” asema Dkt Rita Khamisi, ambaye ni msomi wa historia ya dini.

  • Tags

You can share this post!

Hatari ndani ya mabwawa ya kuogelea

Shirika lazuia watoto kupotea wakiogelea Lamu

T L