• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Hatari ndani ya mabwawa ya kuogelea

Hatari ndani ya mabwawa ya kuogelea

NA MWANGI MUIRURI

MADAKTARI sasa wametoa tahadhari kuhusu mabwawa ya kuogelea ambayo utapata watu wengi wakifurika kupindukia kwa awamu moja wakiwemo watoto.

Wanasema kuna hatari kubwa kuingia kwa mabwawa ya aina hiyo.

Wengi wa wanaomiliki mabwawa hayo wamesutwa kama wanaokimbizana na faida za utozaji ada pasipo kuzingatia viwango vyovyote vya usalama wa kiafya.

“Kitu cha kwanza ni kuelewa kwamba miili yetu huwa michafu ajabu. Iko na viini tele vya magonjwa kwa ngozi. Ajabu ni kwamba, baadhi ya wazazi eti wanaoma raha kuwapeleka watoto wao katika mabwawa ya kulipia na kisha kuwarusha watoto wao ndani kujumuika na makumi ya wengine waogelee. Hiyo ni hatari kubwa,” asema Dkt Leonald Gikera wa Hospitali Kuu ya Murang’a.

Dkt Gikera anasema kwamba “hata hufai kuwa daktari ili kujua kwamba ndani ya mabwawa hayo ya kuogelea kuna baadhi ya watu ambao wanatapika, kukojoa, kumwaga jasho na hata kuenda haja kubwa humo”.

“Taka za aina hiyo ni hatari kwa afya za waogeleaji hao,” akasema.

Naye Dkt Kamau Nginyangi ambaye ni Mkurugenzi wa Afya ya Kidijitali katika Wizara ya Afya, alisema wazazi huruhusu watoto wao waogelee kwa mabwawa ya kuogelea ambapo pia kuna mchanganyiko wa jinsia na pia kuna watoto ambao wameshajua na kujiingiza kwa maswala ya ngono.

Dkt Nginyangi anasema watoto wakubwa na pia baadhi ya watu wazima walio na akili zao,  huingia kwa maji hayo hasa nyakati za usiku na kushiriki ngono, vikiwemo pia vitendo vya ushoga na usagaji.

“Utapata kunao ndani ya maji hayo ambao hata wako na ulevi, wengine wako na hedhi, wengine wako na magonjwa ya ngozi lakini eti kwa sababu wanasaka raha ya kujiachilia kwa msingi wa sherehe za sikukuu, wawaweka wengine hatarini kiafya,” akasema Dkt Nginyangi.

Dkt Nginyangi alisema kwamba kunafaa kuwa na ukaguzi wa mabwawa hayo ya kuogelea yanayotumiwa na umma “lakini hilo ni suala ambalo limetelekezwa na tawala za kaunti ambazo ndizo zinafaa kuweka viwango vya usalama kwa afya ya umma”.

Aliongeza kwamba mabwawa hayo yanafaa kukaguliwa kuhusu utumizi wa dawa za kupambana na viini mbalimbali ili kuyafanya salama, maji hayo kubadilishwa mara kwa mara na kwa kila wakati kuwe na usambamba wa maji kutoka na kuingia humo.

Dkt Stephen Ngigi wa hospitali ya Maragua naye alisema kwamba magonjwa yenye yanaweza yakatoka kwa mabwawa hayo ni kati ya yale ya ngozi hadi saratani.

“Wakati wa kusaka raha, kuna mengi sana ya busara kwa msingi wa afya ambayo sisi hupuuza lakini athari zinapoanza kuingia ikiwemo mauti, ndipo tunaanza kumakinika tukiwa tayari tumechelewa,” akaeleza Dkt Ngigi.

Alisema kwamba “wewe wakati unaingia au unaingiza watoto wako ndani ya kidimbwi cha umma pasipo kwanza kupata hakikisho la viwango vya usafi na pia ukitumia maji hayo mkiwa halaiki ya watu, ujue umetelekeza busara na unapisha hatari kuu kwa maisha yako”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kandanda: Gundi ya mshikamano, silaha dhidi ya mihadarati

Ushoga: Kanisa Katoliki njia panda agizo la Papa likipingwa...

T L