• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Vita Ethiopia vyatishia hali ya Kenya

Vita Ethiopia vyatishia hali ya Kenya

Na MARY WAMBUI

MAPIGANO yanayoendelea nchini Ethiopia yanahatarisha uwekezaji na usalama wa Kenya iwapo hali itaendelea kukuza sintofahamu katika taifa hilo jirani.

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kimataifa, mpango wa kampuni ya Safaricom kuwekeza nchini Ethiopia uko hatarini kusambaratika.

Pia mradi wa LAPSSET ambao unahusisha ujenzi wa Bandari ya Lamu na barabara inayounganisha bandari hiyo na Ethiopia na Sudan Kusini pia uko katika hatari ya kuvurugika.

Kiusalama, machafuko nchini Ethiopia, ambayo yamesambaa hadi eneo la Oromia linalopakana na Kenya, yametajwa kuwa yanayoweza kuchangia ulanguzi wa silaha ambazo zikianguka mikononi mwa majangili, zitakuwa tatizo kwa usalama wa kitaifa.

Wadadisi pia wanahofia kuwa kuhusika kwa makundi ya wapiganaji kutoka Oromia huenda pia kukasababisha wakimbizi kutoka Ethiopia kuingia Kenya.

Safaricom imeanza kutekeleza mipango yake ya kutoa huduma za simu na intaneti nchini humo, lakini sasa mradi huo uko katika hatari ya kuporomoka.

Tayari kundi la wawekezaji kutoka Marekani limechelewesha utoaji wa mkopo wa Sh53.97 bilioni ambao liliahidi kutoa kwa Safaricom katika upanuzi wa huduma zake nchini Ethiopia.

Awali, wawekezaji hao walitishia kujiondoa kwenye mradi huo wakidai ni ukiukaji wa haki za binadamu katika eneo la Tigray.

Wapiganaji wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) wamekuwa wakikabiliana na wanajeshi wa serikali ya Ethiopia kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Serikali ya Kenya imetangaza kuimarishwa kwa doria katika mpaka wa kilomita 800 kati ya Kenya na Ethiopia.

Maafisa wa usalama wa Kenya wameongeza vizuizi barabarani katika juhudi za kuzuia kuingia kwa wakimbizi na silaha haramu humu nchini.

Wataalamu wa masuala ya usalama wameonya kuwa ghasia nchini Ethiopia ni tishio kwa amani katika maeneo yanayopakana na nchi hiyo.

“Kufikia sasa, hakujawa na shughuli zozote za kutiliwa shaka katika mpaka wa Kenya na Ethiopia. Lakini hali ya usalama imeimarishwa na tumejiandaa vyema kupambana na hali yoyote itakayotishia usalama wetu,” Msemaji wa Polisi Bruno, Shioso aliambia Taifa Leo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Upembe wa Afrika, Hassan Khannenje, alisema maelfu ya watu kutoka nchi hiyo jirani huenda wakaingia humu nchini kutafuta hifadhi.

“Mapigano nchini Ethiopia huenda yakasambaa hadi nchini Kenya na kuhatarisha usalama katika maeneo ya mpakani,” akasema Dkt Khannenje.

Mtafiti wa Kujitegemea kuhusu Usalama wa Kitaifa, Bw Edward Wanyonyi, alionya Kenya isipoweka mikakati ya kuzuia mapigano hayo kusambaa, basi italazimika kutumia gharama kubwa.

You can share this post!

Diwani wa Landimawe aafikiana na Nairobi Water kusambaza...

Risala za heri na sifa tele Kibaki akigonga 90

T L