• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wahuni wanaochapisha vitabu feki vya CBC wanyakwa

Wahuni wanaochapisha vitabu feki vya CBC wanyakwa

NA CHARLES WASONGA

MAAFISA wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamenasa watu wawili wakichapisha vitabu feki vya kiada wakilenga kulaghai wazazi walioko kwenye pilkapilka za kununulia wanao vitabu kabla ya shule kufunguliwa Junuari 8, 2024.

Maafisa hao kutoka makao makuu ya DCI wakishirikiana na wenzao kutoka kituo cha polisi cha Central, Jumapili, Desemba 31, 2023 waliwatia nguvuni Christopher Muthini Musyoki na Eugene Asunda ndani ya jengo la Soko Plus, lililoko barabara ya Ronald Ngara wakipiga chapa jalada za kitabu cha “Four Figured Mathematical Tables”.

Wawili hao walifumaniwa katika chumba nambari A36 wakiendesha uhalifu huo.

“Maafisa wa upelelezi vilevile walipiga hatua na kumpata mwajiri wa wawili hao na mmiliki wa mashine hiyo ya kupiga chapa kwa jina, Bw Esikumo Opati. Bw Opati alifichua kwamba alikuwa amepewa kandarasi na Muyela Aluta Samuel ambaye alisakwa na kukamatwa,” DCI ikasema kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya mtandao wa X (awali Twitter).

“Aidha, iligunduliwa kuwa Mayela pia anamiliki biashara ya kupiga chapa katika chumba nambari 9 kilichoko katika jengo la Ruha House katika barabara ya Mfangano. Baada ya upekuzi, mashine ya kupiga chapa na vifaa vya kuchapisha vitabu vya “Four Figured Mathematical Tables” vilipatikana.” DCI ikaongeza.

Baada ya kuhojiwa zaidi, Bw Muyela aliwaelekeza maafisa wa DCI katika duka lililoko katika jengo la Manshram Mansion, chumba nambari 28 katika barabara hiyo ya Mfangano ambako nakala 1, 000 za vitabu hivyo vya “Four Figured Mathematical Tables” visivyo na jalada vilipatikana.

Washukiwa wote katika sakata hiyo wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, Nairobi na watafikishwa kortini mnamo Jumanne, Januari 2, 2024.

DCI imetahadharisha wazazi wanaowanunulia watoto wa vitabu na mahitaji mengine ya shule kuwa makini wakati kama huu wasije wakanaswa kwenye mtego wa walaghai wanaolenga kuwauzia bidhaa ghushi.

 

  • Tags

You can share this post!

Ufanisi dhidi ya pombe haramu Mlima Kenya ilikuwa hekaya tu?

MCA mkarimu Kaunti ya Nairobi

T L